Othman aahidi Chuo Kikuu kumuenzi Maalim Seif

MGOMBEA urais wa Zanzibar kupitia chama cha ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman, ameahidi kuuenzi urithi wa Marehemu Maalim Seif Sharif Hamad kwa kujenga Chuo Kikuu cha Maalim Seif Sharif Hamad katika mji wa Wete, Kaskazini Pemba. “ Chuo hichi kitakuwa ni ngome ya maarifa , uzalendo na maendeleo endelevu kwa vizazi vijavyo,” alisema Masoud.
Akihutubia maelfu ya wafuasi wake kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika kwenye viwanja vya Shule ya Jadida, Othman alisema chuo hicho kitakuwa alama ya heshima na kumbukumbu ya kudumu kwa mchango mkubwa uliotolewa na Marehemu Maalim Seif katika siasa, elimu na maendeleo ya kijamii ya Zanzibar.
“Maalim Seif alikuwa taa ya maarifa, mfano wa uadilifu na nguzo ya umoja wetu. Tunapaswa kumuenzi si kwa maneno tu, bali kwa vitendo vinavyowasha matumaini na kuleta maendeleo. Chuo hiki kitakuwa zawadi ya heshima kwake na urithi kwa kizazi kipya cha Wazanzibari,” alisema Othman huku umati ukilipuka kwa nderemo na vigelegele.
Alifafanua kuwa chuo hicho kitapangwa kwa ubunifu wa kisasa, kikijumuisha vitivo vya elimu, teknolojia, uongozi na sayansi ya jamii, kwa lengo la kuwawezesha vijana wa Zanzibar kupata elimu bora ya juu ndani ya nchi yao.

Othman alisisitiza kuwa chini ya serikali ya ACT Wazalendo, elimu itakuwa nguzo kuu ya maendeleo ya taifa, huku mipango ikiwemo kuimarisha miundombinu ya shule, kutoa mikopo nafuu kwa wanafunzi na kuongeza ajira kwa walimu na wataalamu wa elimu. “Kizazi cha leo hakihitaji ahadi tupu; kinahitaji fursa. Elimu ndiyo silaha ya kupambana na umaskini na utegemezi. Ndiyo maana ujenzi wa chuo hiki ni ahadi ya moyo wangu kwa wananchi wa Zanzibar,” alisema kwa msisitizo.
Wakazi wa Wete na maeneo jirani walipokea tangazo hilo kwa furaha na matumaini makubwa, wakimsifu Othman kwa maono yake ya kuwekeza katika elimu na kumuenzi shujaa wa demokrasia, Marehemu Maalim Seif. Kwa mujibu wa mpango wa awali wa ACT Wazalendo, ujenzi wa Chuo Kikuu cha Maalim Seif Sharif Hamad unatarajiwa kuanza mara tu baada ya uchaguzi.
Awamu ya kwanza itajumuisha majengo ya utawala, maktaba ya kisasa, na vitivo vya elimu, biashara na teknolojia ya habari. Chuo hicho kitakuwa na hadhi ya kimataifa, kikivutia wanafunzi kutoka maeneo yote ya Afrika Mashariki na kutoa nafasi za kubadilishana uzoefu na vyuo vikuu vikubwa duniani.
Viongozi wa ACT Wazalendo walisema mradi huo ni sehemu ya Dira ya Zanzibar Mpya, inayolenga kuimarisha elimu, ajira na ubunifu miongoni mwa vijana. Chuo Kikuu cha Maalim Seif Sharif Hamad kinatarajiwa kupokea zaidi ya wanafunzi 5,000 katika miaka mitano ya mwanzo, kikitumia teknolojia za kisasa katika ufundishaji ili kuandaa wataalamu watakaoipeleka Zanzibar kwenye uchumi wa kidijitali.
Mradi huu unafafanua dhamira ya dhati ya Othman Masoud kujenga Zanzibar yenye elimu, uadilifu na usawa kwa wote. SOMA: Miaka 61 ya Mapinduzi: Kutoka Karume hadi Dk Mwinyi



