Papa Francis aacha zawadi ya jimbo Bagamoyo

ASKOFU Mkuu mstaafu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo amesema Jimbo la Bagamoyo ni zawadi kwa Tanzania iliyotolewa na Papa Francis (88) katika muda wa mwisho wa maisha yake.

Askofu Pengo alisema hayo juzi wakati alipofanya mahojiano na Kituo cha Televisheni cha UTV kuhusu alama iliyoachwa na Papa Francis nchini.

Alisema kutokana na hamu kubwa waliyokuwa nayo Kanisa Katoliki ya kuwa na Jimbo la Bagamoyo walifurahi baada ya Papa Francis kukubali na kubariki kuanzishwa kwa jimbo hilo na hivyo ni kama zawadi kwa Tanzania.

“Amefariki tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwamba katika kipindi chake cha mwisho cha maisha yake ameweza kufanikisha shughuli nzima ambayo tulikuwa na hamu nayo ya kuwa na jimbo la Bagamoyo,” alisema Askofu Pengo.

Papa Francis aliaga dunia Jumatatu wiki hii na anatarajiwa kuzikwa kesho.

Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Dk Charles Kitima alisema Papa Francis alihimiza watu duniani kuishi pamoja na kushirikiana.

“Baba Mtakatifu amehimiza sana katika nyakati hizi tujali sana kuishi pamoja kwa sababu dunia yote ni nafasi ya watu wote kuishi na kushirikiana pamoja,” alisema Dk Kitima.

Wakati huohuo maelfu ya watu wamekusanyika nje ya Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro Mjini Vatican kutoa heshima ya mwisho kwa Papa Francis.

Shughuli hiyo iliyoongozwa na Kardinali Kevin Farrell, ambaye anakaimu nafasi ya Papa hadi pale atakapochaguliwa kiongozi mpya, atasimamia pia shughuli za kutiwa muhuri kwenye jeneza la papa leo na umati wa watu unatarajiwa kuhudhuria tukio hilo.

Mbali na Rais Donald Trump na Volodymyr Zelensky wa Ukraine, viongozi wengine waliothibitisha kuhudhuria mazishi ya kiongozi huyo ni Rais wa Tume ya Umoja wa Ulaya, Ursula Von Der Leyen, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, Rais Frank-Walter Steinmeier na Kansela Olaf Scholz wa Ujerumani.

Rais wa Urusi Vladimir Putin atawakilishwa na Waziri wa Utamaduni, Olga Lyubimova kwa mujibu wa Msemaji wa Ikulu ya Kremlin, Dmitry Peskov.

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button