Papa Francis aomba mapigano kusitishwa kabla ya Krismasi

VATICAN : PAPA Francis ameziomba nchi zinazopigana duniani kusitisha mapigano kabla ya sikukuu ya Krismasi.

Akitoa wito huo katika sala yake ya Jumapili ya wiki hii, Papa alilalamikia mashambulizi ya kikatili yanayoendelea nchini Ukraine na Gaza, akisisitiza kuwa hayo ni mateso makubwa kwa raia wasio na hatia.

“Wacha bunduki zinyamaze na nyimbo za Krismasi zisikie!” alisema Papa Francis, akisisitiza umuhimu wa amani katika kipindi cha sherehe za Krismasi.

Aliendelea kusema, “hebu tuombe kwamba Siku ya Krismasi kuwe na usitishaji wa mapigano katika nyanja zote za vita, nchini Ukraine, katika ardhi takatifu, Mashariki ya Kati na ulimwenguni kote.”

Papa alikumbuka mateso yanayopatikana kwa raia wa Ukraine, ambapo miji inashambuliwa mara kwa mara, huku shule, hospitali, na makanisa yakiharibiwa.

Aidha, alielezea huzuni kubwa aliyonayo kuhusu hali ya Gaza, akielezea jinsi vurugu hizo zinavyohusisha mauaji ya watoto na uharibifu wa taasisi muhimu kama shule na hospitali.

SOMA: Papa asikitishwa na vita Gaza, asema silaha hazileti amani

Wito huu wa Papa Francis unalenga kumaliza machungu na kuteseka kwa raia, huku akisisitiza kwamba Krismasi ni kipindi cha amani na umoja.

 

Habari Zifananazo

Back to top button