JESHI la Polisi mkoani Geita limepokea pikipiki 50 zenye thamani ya Sh milioni 175 kwa lengo la kuimarisha ulinzi na usalama wa kimkakati.
Pikipiki hizo ni kwa ajili ya maofisa wa polisi wakaguzi ngazi ya kata ambao wamekabidhiwa mbele ya Waziri Mambo ya Ndani ya Nchi Mhandisi Hemed Masauni.
Akizungumza baada ya kupokea pikipiki hizo, Mhandisi Masauni ameipongeza Kampuni ya Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGML kwa kutoa pikipiki hizo akisema huo ni mwendelezo wa kuboresha mazingira ya kazi kwa jeshi la polisi nchini.
Amesema serikali inaendelea kuweka mazingira rafiki ya utendaji wa Jeshi la Polisi ambapo kwa mwaka huu wa fedha imetenga Sh bilioni 224 kwa ajili ya miradi ya maendeleo ndani ya jeshi hilo.
Amesema fedha hizo zitatumika kukamilisha, kutekeleza na kuanza ujenzi wa ofisi, vituo na makazi ya askari pamoja na kuongeza vitendea kazi vya kisasa zikiwemo pikipiki, magari na helkopita.
“Hadi sasa tayari tumeshanunua magari 384, kwa ajili ya jeshi la polisi pekee, na siku moja kabla ya Oktoba 20 tulipokea magari 77 kwa Dar es Salaam.
“Magari haya ambayo tumeshaanza kuyapokea yanaenda katika makao makuu ya jeshi la polisi, kwenye ofisi za mikoa, wilaya, na pikipiki zinaenda katika kata, na jumla ya pikipiki 107 zimeshasambazwa,” amesema Masauni.
Amesema pia serikali inaendelea na ujenzi wa majengo ya makao makuu kwenye mikoa 12 ikiwemo mkoa wa Geita ambapo pia inaendelea kushirikiana na wadau ikiwemo GGML kuimarisha usalama.
Mkuu wa Mkoa wa Geita Martine Shigela amesema ujenzi wa jengo la Uhamiaji limeshakamilika huku ujenzi wa jengo la makao makuu ya polisi mkoa unaendelea vizuri.
Meneja Mwandamizi wa Mahusiano GGML, Gilbert Mworia amesema huo ni mwendelezo wa miradi ya kuliunga mkono jeshi la polisi ambapo awali walijenga nyumba sita za maofisa waandamizi wa polisi.
Ofisa wa Polisi Mkaguzi wa Kata wilayani Mbogwe, Edwin Libalio amekiri kuwa kabla ya pikipiki hizo walikuwa wanapitia wakati mgumu kuwafikia wananchi wa vijijini kutokana na mazingira magumu ya barabara.