Polisi Rukwa wakamata vitenge 710 vilivyoingizwa kiholela

JESHI la Polisi Mkoa wa Rukwa limekamata gari aina ya MARK X iliyokuwa imebeba vitenge doti 710 vyenye thamani ya Sh milioni 21 vilivyoingizwa nchini kinyume na sheria, vitenge vilivyokuwa vikisafirishwa kuelekea Mkoa wa Katavi.

Akizungumza na waandishi wa habari Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa ACP Shadrack Masija amesema gari hiyo yenye namba za usajili T.691 CVT aina ya MARK X ilikuwa ikiendeshwa na dereva asiyefahamika ambaye alikimbia baada ya kuwaona askari Polisi.

Amesema ndani ya gari hiyo alikutwa abiria mmoja aitwaye Franco Mwigaga (24) mkazi wa Tunduma na baada ya kufanya uchunguzi walibaini kuwa usajili halali wa gari hiyo ni T. 391 DGW aina ya MARK X ambayo ni mali ya Caroline Salija mkazi wa Dar es Salaam.

Amesema gari pamoja na vitenge vitakabidhiwa ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa hatua nyingine za kisheria.

Aidha ACP Masija ametoa wito kwa wananchi wote wa Mkoa wa Rukwa kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu.

Habari Zifananazo

Back to top button