Polisi wakamata meno ya tembo, nyama ya nyati

JESHI la Polisi mkoani Rukwa limekamata meno ya tembo 11 na nyama ya nyati vipande 56, vyote vikiwa na thamani ya Sh milioni 298.

Kamanda Polisi Mkoa wa Rukwa, Theopista Mallya aliyasema hayo wakati alipozungumza na waandishi wa habari jana.

Alisema nyara hizo za serikali zilikamatwa kutokana na operesheni na misako mbalimbali iliyofanyika katika kipindi cha Januari hadi Novemba 2022.

Akifafanua alisema katika operesheni na misako hiyo pia zilikamatwa silaha nane zilizotengenezwa kienyeji na risasi 75 za shotgun na tatu za riffle.

Pia katika kipindi hicho zilikamatwa lita 4,266 za pombe ya moshi, mitambo 42 ya kutengeneza pombe hiyo, bangi kilogramu 17 na gramu 854 na mashamba ya bangi yenye ukubwa wa ekari 8.5.

Alisema kutokana na elimu iliyotolewa na jeshi hilo katika usalimishaji wa silaha kwa hiari zilizokuwa zinamilikiwa kinyume na utaratibu, silaha 17 zilisalimishwa katika vituo vya polisi.

Lakini pia silaga nyingine 49 zilikamatwa katika matukio mbalimbali na kihifadhiwa vituo vya polisi.

Katika hatua nyingine, alisema waganga 189 wanaopiga ramli chonganishi maarufu lambalamba wamefikishwa mahakamani huku kesi tatu zikiwa katika hatua ya upelelezi na zikikamilika watuhumiwa watafikishwa mahakamani.

Habari Zifananazo

Back to top button