JESHI la Polisi limesema limeanza uchunguzi kutambua chanzo cha kifo cha Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Nusura Hassan Abdallah kilichotokea mkoani Kilimanjaro.
Taarifa iliyotolewa leo na Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, David Misime imeeleza kuwa taarifa za kifo cha mwanafunzi huyo zimekuwa zikihusisha ajali iliyotokea Jijini Dodoma Aprili 26, 2023 ikimhusisha Naibu Waziri TAMISEMI, Dk Festo Dugange lakini pia taarifa nyingine zinadai kifo chake kimetokana na kipigo kutoka kwa Mpenzi wake.
“Jeshi la Polisi lingependa kutoa ufafanuzi kuwa, Polisi Mkoa wa Kilimanjaro baada ya kuona taarifa hizo kupitia mitandao ya kijamii na sababu zinazotolewa, wameshaanza uchunguzi kwa watu mbalimbali, Hospitali alikotibiwa binti huyo ambapo na wanashirikisha Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) na wadau wengine wa haki jinai.” Imeeleza taarifa hiyo.
Aidha Jeshi hilo limetoa wito kwa mtu yoyote mwenye taarifa zilizosahihi na zenye ukweli asisite kuwapa Polisi taarifa hizo ili kuharakisha uchunguzi wa tukio hilo.
“Uchunguzi wa tukio hilo ukikamilika taarifa kamili ya kilichobainika itatolewa kwa umma kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za nchi.” Imefafanua taarifa.