POLISI mkoani Morogoro inamshikiria Subira John ,25, mkulima mkazi Mtaa wa Mtendeni, Kata ya Mkwatani, Wilaya ya Kilosa kwa tuhuma za kutelekeza mtoto mchanga.
Kamanda wa polisi wa mkoa huo, Alex Mkama amethibitisha kutokea kwa tukio hilo leo Desemba 4, 2024 na kuongeza kuwa mtuhumiwa alikamatwa Desemba 2, 2024 akiwa kajificha kwenye nyumba ya wageni isiyo na jina maarufu ‘Gesti Bubu’.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa mkoa tukio la kutekelezwa kwa mtoto huyo mchanga lilifanyika Novemba 8,2024 majira ya mchana katika eneo la K Park bar kitongoji cha Mbumi, Kata ya Mbumi, Wilaya ya Kilosa.
“Mtuhumiwa huyo anadaiwa alimfukia mtoto mchanga huyo mwenye umri wa siku moja jinsia ya kiume na kuacha kichwa nje ya shimo na kutoroka kusikojulikana,” amesema Mkama.
Mkama amesema baadayae zilisambaa taarifa za utelekezwaji wa mtoto mchanga, polisi ilianza uchunguzi ili kubaini mtuhumiwa wa tukio hilo, baada ya ufuatiliaji Desemba 2, 2024 mtuhumiwa huyo alikamatwa akiwa kajificha kwenye nyumba ya wageni hiyo.
Amesema polisi kwa kushirikiana na taasisi nyingine ikiwemo ustawi wa jamii walifanikiwa kumchukua mtoto mchanga huyo na kumpeleka katika kituo cha kulelea watoto cha Msista Mgolole kilichopo Kata ya Bigwa, Manispaa ya Morogoro, Mkoa wa Morogoro.
“ Kwa sasa mtoto huyo mchanga anaendelea vizuri na upelekezi unaendelea kukamilishwa kwa ajili ya hatua nyingine za kisheria,” amesema Mkama.
Kutokana na tukio hilo la ukatili dhidi ya watoto ametoa wito kwa wananchi kuacha tabia ya kutelekeza watoto wachanga na badala yake wawalee kwani hilo ni taifa la kesho.