TFS wataka ulinzi ubora wa asali

TABORA: WANANCHI wanaojihusisha na ufugaji nyuki na uchakataji wa mazao yatokanayo na nyuki wametakiwa kuzingatia viwango vya ubora na usalama wa bidhaa zao, kwani uzalishaji usiozingatia sheria unaweza kuhatarisha masoko ya ndani na nje ya nchi.
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Hussein Msuya, amesema hayo wakati wa majadiliano ya biashara kwa biashara na mdahalo kuhusu maendeleo ya sekta ya ufugaji nyuki nchini.
Mdahalo huo uliofanyika katika viwanja vya Kumbukumbu ya Vita mkoani Tabora Maadhimisho ya Siku ya Nyuki Duniani ambayo kitaifa yalifanyika mkoani humo.
Msuya ambaye pia ni Meneja wa Rasilimali za Nyuki TFS amesema Tanzania imeendelea kujijengea sifa kimataifa kutokana na ubora wa mazao yake ya nyuki, hususan asali na nta.
Amesema ubora huo unaweza kupotea iwapo wafugaji na wachakataji wa mazao ya nyuki hawatazingatia viwango vilivyowekwa na mamlaka husika.
“Utumiaji wa vifungashi bora ni takwa la kisheria na unasimamiwa na sheria ya viwango. Kwa mujibu wa kanuni za ufugaji nyuki, asali lazima ifungashwe kwa ubora na iwekwe lebo kwa mujibu wa Kanuni ya 21 ya ufugaji wa nyuki,” amesema Msuya.
Msuya amesema baadhi ya changamoto zinazoikabili sekta hiyo ni pamoja na matumizi ya vifungashio visivyokidhi viwango, uchakataji usiozingatia usafi pamoja na uhifadhi usiofaa wa bidhaa za nyuki, hali inayoweza kushusha ubora wa bidhaa na kupunguza imani ya wanunuzi.
Hivyo amewataka wananchi kutumia vifaa sahihi wakati wa uvunaji na uchakataji wa asali, nta na gundi ya nyuki ili kuhakikisha bidhaa hizo zinadumu katika ubora unaokubalika kwenye soko la ushindani.
“Wito wangu kwa wananchi ni kujikita katika matumizi ya vifungashio vilivyoidhinishwa na vinavyokidhi viwango vya ubora na usalama wa asali,” amesisitiza Msuya
Kwa upande wao, baadhi ya washiriki wa mdahalo huo akiwemo Mwenyekiti wa Kikundi cha Miombo kutoka wilaya ya Sikonge , Damson Moses ,waliishukuru TFS kwa kuendelea kutoa elimu ya ufugaji bora wa nyuki, wakisema mafunzo hayo yatawawezesha kuongeza uzalishaji wa bidhaa zenye ubora na kuongeza kipato cha kaya zao.



