Polisi yamsaka mwanamke aliyeiba mtoto wa siku moja

MTOTO mchanga mwenye umri wa siku moja ameibiwa katika Kata ya Buzuruga, Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Mwanza, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza Wilbrod Mutafungwa alisema tukio hilo lilitokea Februari 7, mwaka huu majira 10:00 jioni Buzuruga katika Manispaa ya Ilemela.

Alisema Februari 6, mwaka huu, mkazi wa Mtaa wa Nyasaka – Msumbiji, Nice Renatus (24) alikwenda katika Kituo cha Afya Buzuruga kujifungua na alijifungua salama mtoto wa kike na kupewa mapumziko katika chumba Na.4 kilicho katika kituo hicho cha afya.

Alisema akiwa amepumzika kituoni hapo alikwenda hapo mwanamke mmoja ambaye jina lake halikufahamika mwenye umri kati ya miaka 35 au 40 na kujitambulisha kuwa ni mke wa mjomba wake na alikwenda kwa ajili ya kumuona mwanamke huyo aliyekuwa amejifungua.

“Alimpatia huduma mbalimbali ikiwa ni pamoja na kumpatia chai,” alisema.

Alisema ilipofika Februari 7, mwaka huu majira ya saa 11:00 jioni Nice akiwa na mtoto wake aliruhusiwa kutoka hospitali baada ya hali yake ya kiafya kuimarika na wakati anaondoka hospitalini hapo kuelekea nyumbani ndipo mwanamke huyo ambaye awali alijitambulisha kuwa ni mke wa mjomba wake alimuomba amsaidie kubeba mtoto huyo kwenda nyumbani.

“Wakiwa njiani alimpitisha vichochoroni hadi kwenye nyumba ambayo alidai kuwa ni nyumba yake.

Alizunguka nyumba akidai anatafuta funguo ili waingie ndani kisha akatoweka na mtoto kuelekea kusikojulikana,” alifafanua.

Kamanda Mutafungwa alisema mama mzazi wa mtoto alibaki nje ya nyumba hiyo hadi alipoanza kutiliwa wasiwasi na familia ambayo ni wamiliki halali wa nyumba hiyo ndipo ikabainika kuwa mama huyo alikuwa ameibiwa mtoto wake mwenye umri wa siku moja na taarifa ikafikishwa kituo cha polisi.

“Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza, linaendelea kufanya uchunguzi wa kina kuhusiana na tukio hilo ili kubaini chanzo cha tukio hilo na kumkamata mwanamke huyo ambaye amefanya tukio la wizi wa mtoto,” alisema.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button