Makalla aipongeza AICC kwa huduma ya Utalii wa Mikutano

MKUU wa Mkoa wa Arusha CPA Amos Makalla ameipongeza Menejimenti na wafanyakazi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC) kwa mchango wake katika kukuza Utalii wa Mikutano na kuwezesha mkutano wa kimataifa wa Nchi 120 uliofanyika hivi karibuni, akisema anaamini kuwa kituo kimejipanga kuhudumia Bunge la IPU litakalofanya mkutano wake October mwaka huu jijini Arusha.

Makalla ametoa pongezi hizo leo Februari 06, 2026, wakati wa Kikao cha kawaida cha Baraza la Wafanyakazi wa kituo hicho, akisema AICC imekuwa na mchango mkubwa pia katika kuutangaza Mkoa wa Arusha na Tanzania Kimataifa na kutaka kila mtumishi kuwajibika ipasavyo katika kutimiza malengo na maono ya serikali katika Kituo hicho.

Amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuboresha utoaji wa huduma ikiwa ni pamoja na huduma za ukarimu na itifaki pamoja na kujikita katika matumizi ya teknolojia ili kuendelea kuvutia zaidi kufanyika kwa mikutano katika kituo hicho pamoja na kujiandaa na fursa zitakazokuwepo wakati wa Michuano ya Soka ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2027), baadhi ya michezo ikichezwa Jijini Arusha.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa Kituo hicho Christine Mwakatobe amesema AICC kwa sasa ina ithibati ya kimataifa katika sekta ya mikutano duniani, akisema mpango wao ni kuhakikisha wanaendelea kuboresha zaidi utoaji wa huduma na matumizi ya teknolojia kituoni hapo.

Amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa msukumo wake na jitihada zake za kukuza diplomasia na mahusiano ya Kimataifa pamoja na kuimarisha amani, usalama na utulivu nchini.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button