Polisi yasikitishwa adhabu kali mashuleni, majumbani
ADHABU kali zilizopitiliza kutoka kwa walimu na walezi ni sehemu ya matukio ya ukatili wa kijinsia kwa wanafunzi yaliyolilazimisha jeshi la Polisi kutoa elimu ya kukabiliana na vitendo hivyo mashuleni.
Akitoa elimu kwa wanafunzi wa shule ya Msingi Azimio ya mjini Iringa, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, ACP Allan Bukumbi alisema; ” Tumelazimika kuja mashuleni baada ya kuona kuna ongezeko la matukio mbalimbali ya ukatili kwa watoto.”
Kwa kushirikiana na taasisi na wadau mbalimbali alisema jeshi la Polisi litaongeza nguvu katika kupunguza vitendo hivyo na kuchukua hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kuwafikisha mahakamani wahusika wake wote.
Alisema shule ya msingi Azimio ni moja ya shule zenye changamoto ya wanafunzi kujihusisha na matukio ya kiuhalifu kama utoro, wizi na vitendo vya ngono jambo linalowafanya baadhi ya wazazi, walezi na hata walimu wake wawape adhabu kali kinyume na sheria.
Alitoa wito kwa wazazi kuongeza usimamizi wa karibu kwa watoto wao ili kuwaepusha na matukio hayo na walimu kuongeza bidii ya ufundishaji na kutoa adhabu kwa kuzingatia miongozo na taratibu zilizowekwa kisheria.
Mratibu wa Elimu Kata wa Kata ya Mshindo, Eva Ndunguru alisema katika shule hiyo kumekuwepo na matukio ya watoto wengi kulalamika kupewa adhabu kali ya kuchomwa moto mikononi na wazazi au walezi wao kwasababu ya makosa mbalimbali wanayofanya.
Aidha alisema wanafunzi wengine wanalalamika kujilea wenyewe kwa kile kinachoonekana wazazi au walezi kutotimiza wajibu wao na hivyo kuathiri kwa kiwango kikubwa maendeleo yao kitaaluma.
Katika kushughulikia changamoto hiyo na zingine zinazohusiana na ukatili wa kijinsia kama vile kufanyiwa vitendo vya ngono kama ubakaji na ulawiti, kutelekezwa na kutopewa mahitaji muhimu na kukatishwa masomo, ACP Bukumbi aliwataka wananchi kuendelea kutoa taarifa kwa jeshi hilo ili wahusike wakamatwe na washughulikiwe kisheria.
“Kuna baadhi ya jamii watoto wanapewa adhabu kali mashuleni na majumbani zinazosababisha wapate madhara makubwa ya kimwili kama ulemevu wa kudumu, kuathirika kisaikolojia na kukosa uwezo wa kuendelea na masomo. Hilo ni kosa,” alisema.
Aidha Jeshi la Polisi limesema ni kosa kisheria kwa watoto kucheza michezo ya bahati nasibu huku likiwataka walezi na wazazi wasiwaache watoto wakitembea usiku bila kuchukua tahadhari pamoja na kuwahusisha na biashara katika maeneo ya starehe kama vile vilabuni.