JESHI la Polisi nchini limesema ajali iliyotokea Aprili 26, 2023 ikimuhusisha Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI Dk Festo Dugange ilisababishwa na Bodaboda aliyekuwa akivuka barabara ghafla bila kuchukua tahadhari.
Taarifa ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, ACP Martin Otieno imesema gari hilo lenye usajili wa T 454DWV aina ya Toyota Land Cruiser likiendeshwa na Naibu Waziri Dugange lilipoteza mwelekeo na kugonga kigo ya barabara ya Iyumbu maeneo ya St Peter Clever na kupinduka.
“Kulikuwa na mtu moja tu (dereva) kwenye gari hilo ambaye ni Naibu Waziri. Alivunjika kidole gumba cha mkono wa kulia na kupata majeraha katika mkono huo,” amesema Kamanda Martin katika taarifa iliyochapishwa na TAMISEMI.
Makamu wa Rais Dk Philip Mpango amemjulia hali Dk Ndugage ambaye amelazwa katika Hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Doodma.
Jeshi la Polisi limekanusha uvumi kuwa kulikuwa na Mwanamke katika gari hiyo ambaye jina lake halijafahamika na kwamba alipoteza maisha. Halikufafunua sababu ya gari hilo kuonekana katika eneo tofauti na kituo cha polisi kama ilivyo kawaida ya magari yanayopata ajali na kuondolewa na askari wa usalama barabarani.
“Nipende kutoa rai kwa wananchi kuacha kusambaza taarifa za uongo na kuzua taharuki kwa watu bila ya kufanya utafiti,” amesema na kuongeza kuwa “Jeshi la Polisi liko macho na makini kufuatilia na kutoa ufafanuzi wa taarifa zozote.”