Polisi yawatahadharisha Chadema
DAR ES SALAAM — Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewataka viongozi wa CHADEMA kuacha mara moja kampeni ya kuhamasisha wafuasi wao kufika Mahakama ya Kisutu Aprili 24, wakati ambapo Tundu Lissu anatarajiwa kufikishwa mahakamani.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema “kuna dalili za wazi za mipango ya kufanya vurugu” na kwamba lengo ni kuishinikiza mahakama kupitia nguvu ya umma — jambo alilolieleza ni kinyume cha sheria.
“Mahakama ni chombo huru, kinapaswa kuheshimiwa,” alisema Kamanda Muliro, akiongeza kuwa polisi wataimarisha ulinzi katika maeneo yote muhimu jijini, hususan Kisutu, ili kuhakikisha utulivu unadumu.
Muliro pia amewaonya wote watakaoshiriki katika mkusanyiko huo haramu kuwa “hatua kali zitachukuliwa,” na akawahimiza wakazi wa jiji kuendelea na shughuli zao za kila siku bila hofu.



