PPP nguzo ya utekelezaji Dira 2050

NI asubuhi yenye upepo mwanana katika viunga vya Chuo Kikuu Katoliki cha Ruaha (RUCU) mkoani Iringa.
Ndani ya ukumbi wa mikutano, wasomi, wachumi na wadau wa maendeleo wameketi kwa makini katika kongamano la kujadili mustakabali wa Tanzania kuelekea mwaka 2050.
Kaulimbiu ya kongamano hilo lililoandaliwa kwa ushirikiano wa RUCU na Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPPC) likiwa limebeba matumaini makubwa ni ‘Je, Tunakwenda Kuelekea Uchumi Jumuishi?’
Ni mjadala wa kitaifa unaogusa si tu namba na takwimu, bali pia maisha ya kila Mtanzania. Mchumi mashuhuri, Profesa Samwel Wangwe anasema Tanzania haiwezi kufikia uchumi jumuishi bila mageuzi makubwa ya kimuundo katika sekta muhimu kama kilimo, viwanda na usafirishaji.
“Ili kufikia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, tunapaswa kuimarisha sekta ya usafirishaji na kuiweka Tanzania katika nafasi ya kuwa kitovu cha nchi zisizo na bandari,’ anasema Profesa Wangwe. Anaongeza: “Tunapaswa kuzipa kipaumbele sekta zinazounganisha viwanda, kuunda ajira na kutoa fursa za mapato ya muda mrefu”.
Anasisitiza pia umuhimu wa utawala bora na uwajibikaji katika ngazi zote za serikali. Profesa Wangwe anasena maendeleo jumuishi hayawezi kupatikana kama serikali za mitaa hazitaelewa wajibu zilionao katika kupambana na rushwa na kuboresha huduma kwa wananchi.
SOMA: Kafulila ataka PPP ya ufanisi Dira 2050
Kwa mtazamo wake, suluhisho mojawapo ni kuimarisha ushirikiano kati ya sekta ya umma, binafsi na jamii. “Ushirikiano huo,” anasema ndio utakaowawezesha wananchi hasa wanawake na vijana kushiriki kikamilifu katika kupanga na kutekeleza miradi ya maendeleo.
Makamu Mkuu wa RUCU, Profesa Sista Chrispina Lekule anasema hakuna mabadiliko ya kweli bila uwekezaji thabiti katika rasilimaliwatu. “Elimu ni injini ya mabadiliko. Bila elimu bora, hatuwezi kufikia Dira ya 2050 kwa kuwa tunahitaji raia wenye ujuzi, ubunifu na uwezo wa kubadilika ili kuharakisha ukuaji wa uchumi,” anasema Profesa Sista Lekule.
Anaongeza kuwa, vyuo vikuu vinapaswa kufanya mageuzi ya mitaala na kujikita zaidi katika utafiti wenye matumizi ya moja kwa moja, ubunifu na ujasiriamali. Kwa mujibu wa Profesa Sista Lukule, ushirikiano kati ya vyuo na sekta binafsi unaweza kuwa kichocheo cha maendeleo ya teknolojia na ajira kwa vijana.
Katika kongamano hilo, Profesa Humphrey Moshi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) anasema maendeleo hayaji bila kuwapo na haki na amani. “Kudumisha amani na utulivu kutatuwezesha kusonga mbele; tunapaswa kulinda amani na utulivu tulionao,” anasema.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPPC), David Kafulila anasisitiza kuwa sekta binafsi ndiyo injini ya uchumi wa taifa. Anasema biashara ndogo na za kati nyingi zikiwa zinamilikiwa na wanawake na vijana, zinapaswa kupewa nafasi kubwa zaidi.
“SMEs (biashara ndogo na za kati) ni uti wa mgongo wa uchumi wetu. Ili kufikia uchumi wa trilioni moja ya Dola ifikikapo mwaka 2050, tunapaswa kujenga mazingira rafiki kwa biashara zinazoongozwa na wananchi kukua na kustawi,” anasema.
Kafulila anabainisha mafanikio makubwa katika sekta mbalimbali zikiwemo za wachimbaji wadogo kuongeza mchango katika mapato ya madini kutoka asilimia 20 mwaka 2021 hadi asilimia 40 mwaka 2025. Aidha, anasema mapato ya utalii yamepanda kutoka Dola bilioni 1.3 mwaka 2021 hadi bilioni 4 mwaka 2025 na kwamba, zaidi ya Watanzania milioni 1.5 sasa wanapata ajira katika sekta ya utalii.
Kwa mujibu wa Kafulila, eneo la kilimo cha umwagiliaji limeongezeka kutoka hekta 500,000 mwaka 2021 hadi hekta 980,000 mwaka 2025, huku biashara za kimataifa zikiongezeka kutoka Dola za Marekani bilioni 17 hadi 34.
Hata hivyo Kafulila anaweka wazi kuwa, PPP si ubinafsishaji kama wengi wanavyodhani. “PPP si ubinafsishaji; serikali inabaki mmiliki wa mali huku sekta binafsi ikileta mtaji, utaalamu na teknolojia,” anasema. Anaongeza: “Mfano mzuri ni Bandari ya Dar es Salaam, ambako mfumo huu unatekelezwa kwa mafanikio na unatarajiwa kupanuliwa hadi Bagamoyo na Tanga”.
Baadhi ya washiriki wa kongamano hilo wanasema mfumo wa PPP unapaswa kupanuliwa hadi kwenye serikali za mitaa. Wanasema halmashauri zinaweza kutumia ubia huo kujenga masoko, maegesho, miradi ya umwagiliaji na huduma nyingine za kijamii.
Kwamba hatua hiyo itapunguza mzigo wa kifedha kwa serikali na kuongeza tija katika utoaji wa huduma kwa wananchi. Mfanyabishara, Profil Mlawa anasema mafanikio ya Dira ya Maendeleo 2050 hayawezi kupatikana bila uwazi, uwajibikaji na mapambano makali dhidi ya rushwa.
Anasema wananchi wanapaswa kushirikishwa kikamilifu katika miradi ya maendeleo ili kuelewa na kufuatilia manufaa ya ubia huo kwani wengine hawafahamu. Mlawa anabainisha, “PPPC imekuwa na miradi mingi ambayo tayari mafanikio yake yameonekana kama DDC, UDART na bandari. Hili sasa linapaswa kuendelea kuelimisha jamii na kushirikisha zaidi sekta binafsi kwa kila hatua.”
Anaendelea, “Wakifanya hivi tutaweza kufikia malengo tunayoyataka”. Mmoja wa washiriki wa kongamano hilo, Gwantwa Mwakyusa anafurahia uwepo wa miradi inayotekelezwa chini ya PPP akisema ni ishara tosha inayoangazia mafanikio ya mbeleni ya kutekekeleza miradi mingi inayoainishwa na PPPC.
Anasema kilimo kama uti wa mgongo wa uchumi wa taifa ndiyo njia rahisi zaidi ya kujenga uchumi jumuishi kama kitaunganishwa na teknolojia, utafiti na viwanda vya kuongeza thamani ya mazao. Anasema, “Teknolojia na ubunifu ni injini ya mageuzi ya uchumi. Serikali na sekta binafsi zinapaswa kuwekeza zaidi katika tafiti na ujasiriamali wa vijana.”
Kauli za wachumi, wasomi na watendaji wa maendeleo zinaunganika katika ujumbe mmoja: Kufikia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 si ndoto ikiwa Tanzania itaimarisha ushirikiano wa kweli kati ya serikali, sekta binafsi na wananchi. Ubia wa Sekta ya Umma na Binafsi (PPP) si tu chombo cha kifedha, bali ni daraja la kuunganisha nguvu za Watanzania wote kuelekea uchumi jumuishi, shindani na endelevu.
“Mafanikio ya Dira ya 2050 hayatazaliwa kwenye makaratasi ya sera pekee, bali kwenye vitendo vya ubia, ubunifu na uwajibikaji wa kila raia,” anasema Mwakyusa. Mkurugenzi wa Miradi wa PPPC, Agustino Saibul anasema
ipo miradi zaidi ya 80 iliyo chini ya PPP ambayo iko katika hatua tofauti za utekelezaji na mingine imeshatekelezwa.