PURA yaikaribisha Chevron Tanzania kuwekeza sekta ya mafuta, gesi asilia

ACCRA, GHANA: Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) imeikaribisha moja ya kampuni kubwa ya nishati ya Marekani ijulikanayo kama Chevron Corporation kuwekeza katika shughuli za mkondo wa juu wa petroli nchini Tanzania.
PURA imeikaribisha kampuni hiyo wakati wa Wiki ya Mafuta Afrika 2025 iliyofanyika hivi karibuni Jijini Accra, Ghana kupitia kikao kilichohudhuriwa na viongozi na maafisa waandamizi kutoka pande zote akiwemo Mkurugenzi Mkuu wa PURA Mhandisi Charles Sangweni na Meneja anayeshughulika na utafutaji wa mafuta na fursa mpya kutoka Chevron, Jan Pluis.
Katika kikao hicho, Sangweni aliijulisha Chevron kuhusu fursa zilizopo nchini Tanzania zinazotokana na shughuli za utafutaji, uendelezaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia na mipango iliyopo ikiwemo uzinduzi wa duru ya tano ya kunadi vitalu vya utafutaji wa mafuta na gesi asilia.
“Ukizingatia kwamba ni takribani asilimia 30 pekee yamiamba tabaka iliyopo Tanzania ndio imefanyiwa utafiti wa mafuta na gesi asilia, na kwa kuzingatia mipango iliyopo ya kuvutia uwekezaji ikiwemo mapango wa kunadi vitalu vya utafutaji wa mafuta na gesi asilia unaotarajiwa kufanyika, Tanzania ina fursa nyingi kwa Chevron kuwekeza” alisema Sangweni.
Aliongeza kuwa, uwepo wa vitalu vinavyozalisha gesi asilia na miundombinu ya kuchakata na kusafirisha gesi asilia nchini kunaifanya Tanzania kuwa eneo la kimkakati kwa Chevron kuwekeza.
SOMA: PURA, ALNAFT wakutana Algiers kujadili namna ya kinua sekta ya gesi asilia
Kwa upande wake, Pluis alieleza kuwa Chevron imejidhatiti na imedhamiria kuendeleza uwekezaji wake Barani Afrika, akirejea uwekezaji wa kampuni hiyo katika nchi mbalimbali Afrika zikiwemo Nigeria, Equatorial Guinea na Angola.
Aidha, alieleza kuwa, kutokana na fursa zilizopo, Chevron inaitazama sekta ya mafuta na gesi asilia ya Tanzania kwa shauku kubwa na kampuni hiyo imeendelea kuweka mikakati ya kutumia fursa zilizopo katika sekta ya mafuta na gesi asilia nchini Tanzania.