PURA yakoshwa ufadhili wa matibabu ya magonjwa yasiyopewa kipaumbele

"Kwa niaba ya PURA nitumie fursa hii kuipongeza kwa dhati Kampuni ya Equinor Tanzania kwa kufadhili upasuaji huu. Kwa hakika mradi huu unabadilisha maisha ya wagonjwa na tumeguswa sana na mchango wa Equinor katika eneo hili," aliongeza Mollel.

LINDI: Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) imeipongeza kampuni ya nishati ya Kimataifa ya Equinor Tanzania AS kwa kufadhili programu ya taifa ya magonjwa yasiyopewa kipaumbele (NTD).

Hadi sasa kampeni hiyo umesaidia jumla ya wagonjwa wapatao 1,600 kufanyiwa upasuaji wa ngiri maji na ngiri kokoto.

Pongezi hizo zimetolewa leo, Oktoba 6, 2023, mkoani Lindi mara baada ya PURA kutembelea kambi hiyo maalum ya upasuaji wa ngiri maji na ngiri kokoto katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Lindi ya Sokoine.

Akitoa maelezo kwa maofisa wa PURA waliofika kambini hapo, mmoja wa maofisa wa Equinor Tanzania, Dk Naomi Makota amesema kuwa kambi ya upasuaji kwa mwaka huu ilianza Oktoba 2, 2023 na itahitimishwa Oktoba 13, 2023.

Mwaka huu, kampeni hiyo imelenga kuwafikia  wagonjwa 200 kutoka Halmashauri za Lindi na Mtama.

Dk Naomi ameeleza kuwa huu ni mwaka wa tisa tangu Kampuni ya Equinor (iliyokuwa ikijulikana kama Statoil) ianze kufadhili Programu ya NTD ili kuwafanikisha upasuaji wa wagonjwa hao.

Mradi huu kwa Equinor ulianza mwaka 2015 mkoani Mtwara na baadae Lindi mwaka 2017 mpaka leo hii.

Kwa mujibu wa Dk Naomi, tangu kuanza kwa utekelezaji wa programu hii, zaidi ya wagonjwa 1,600 wa ngiri maji na ngiri kokoto wamefanyiwa upasuaji.

Mradi huu hadi sasa umegharimu takribani Dola za Marekani 424,400.

Akizungumza mara baada ya kujionea utekelezaji, ofisa wa PURA, Ebeneza Mollel ameipongeza kampuni ya Equinor Tanzania kwa kurudisha tabasamu kwa wagonjwa wa ngiri maji na ngiri kokoto, kupitia mradi huu muhimu.

“Kwa niaba ya PURA nitumie fursa hii kuipongeza kwa dhati Kampuni ya Equinor Tanzania kwa kufadhili upasuaji huu. Kwa hakika mradi huu unabadilisha maisha ya wagonjwa na tumeguswa sana na mchango wa Equinor katika eneo hili,” aliongeza Mollel.

Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) ni taasisi ya Serikali iliyoanzishwa kupitia Kifungu Namba 11 cha Sheria ya Petroli ya mwaka 2015 kwa lengo la kudhibiti shughuli za utafutaji, uendelezaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia nchini.

Habari Zifananazo

Back to top button