PURA yashiriki ukaguzi, majaribio mtambo kuchimba gesi asilia

Tianjin, China: Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) imeshiriki zoezi la ukaguzi na majaribio ya mtambo utakaotumika kuchimba visima vitatu vya gesi asilia katika Kitalu cha Mnazi Bay mkoani Mtwara.
Zoezi hilo lililofanyika katika Jimbo la Tianjin nchini China, ulilenga kuhakiki uimara na ufanisi wa mtambo huo kabla ya kusafirishwa kuja nchini tayari kuanza mradi wa uchimbaji wa visima vya gesi asilia vitatu unaotarajiwa Novemba, mwaka huu.
Pamoja na ukaguzi wa mtambo huo wenye uwezo wa kuchimba hadi urefu wa mita 8,000, PURA pia ilishiriki kama mtazamaji katika ukaguzi na majaribio ya mifumo mbalimbali iliyopo katika mtambo huo na mabomba yatakayotumika wakati wa uchimbaji.
SOMA: PURA yaja na mikakati upatikanaji wa gesi asilia nchini
Hatua hii ya ukaguzi ni muhimu kwani wataalam hupata fursa ya kujiridhisha juu ya ufanisi wa mtambo kabla ya kuanza kwa utekelezaji wa mradi.
PURA, kama mdhibiti wa shughuli za mkondo wa juu wa petroli nchini inashiriki na kusimamia hatua zote za mradi kuhakikisha mradi unatekelezwa kama ulivyopangwa.
Inatarajiwa kuwa, visima vitakavyochimbwa (MS-2, MB-5 na Kasa-1x), vitaongeza uzalishaji wa gesi asilia kwa zaidi ya futi za ujazo milioni 30 kwa siku.