QNET kuchunguza waliotapeli kwa jina lake

DAR ES SALAAM: KAMPUNI ya kimataifa ya QNET imesema iko tayari kushirikiana na mamlaka husika kuchunguza watu wanaodaiwa kutumia jina lake kuwalaghai vijana 125 kutoka mikoa 11 nchini kwa ahadi za ajira na mafanikio ya haraka ya kifedha mkoani Singida.
Meneja Mkuu wa QNET Kanda ya Afrika Mashariki na Kusini, Jared Thwaits, amesema kampuni hiyo inataka kubaini watu waliohusika, uhusiano wao na kampuni pamoja na iwapo walikuwa na mamlaka ya kuiwakilisha.
Hatua hiyo inafuatia taarifa za vijana hao kudaiwa kushawishiwa kutoa fedha kwa ahadi za kupata ajira na kujipatia mafanikio ya kifedha kwa muda mfupi. Baadhi yao pia wanadaiwa kuishi katika mazingira yasiyofaa, hali iliyosababisha mamlaka za eneo hilo kuingilia kati.
Thwaits amesema QNET imesikitishwa na madai hayo kutokana na madhara yanayoweza kuwakumba vijana na familia zao, huku akisisitiza kuwa kampuni hiyo inapinga udanganyifu na unyonyaji wa kifedha.
Amesema watu wanaodaiwa kuendesha shughuli hizo kwa kutumia jina la QNET si Wasambazaji Huru waliosajiliwa na kampuni hiyo, hivyo uhusiano wao na kampuni unahitaji kufahamika kupitia uchunguzi.
“Ni lazima tubaini nani anahusika, uhusiano wao halisi ni upi, na kama walikuwa wameidhinishwa kuiwakilisha kampuni. Madai ya vitendo visivyo halali lazima yafanyiwe uchunguzi wa kina, na uwajibikaji unapaswa kutegemea ukweli uliothibitishwa,” amesema Thwaits.
Ameeleza kuwa mfumo wa biashara wa QNET unategemea mauzo ya bidhaa kupitia Wasambazaji Huru, na si kuuza nafasi za ajira au kuahidi watu mapato ya uhakika. Pia amesema kampuni hiyo hairuhusu watu kukusanya fedha kwa kutumia jina lake kwa ahadi za ajira au utajiri wa haraka.
Aidha, Thwaits amesema kampuni hiyo iko tayari kutoa ushirikiano kwa mamlaka zinazochunguza tukio hilo ili kusaidia kubaini ukweli na kuhakikisha hatua stahiki zinachukuliwa dhidi ya watakaobainika kuhusika. Amewataka wananchi kuthibitisha uhalali wa fursa zinazotolewa na watu wanaodai kuiwakilisha QNET kupitia njia rasmi kabla ya kufanya malipo au kuingia katika makubaliano ya kibiashara.



