Raha za Yanga hadi bungeni
DODOMA; YANGA juzi ilitwaa ubingwa wa michuano ya Kombe la Shirikisho la CRDB pale Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar kwa penalti 6-5 dhidi ya Azam FC katika mchezo wa fainali ya michuano hiyo.
Kama ulikuwa unafikiri jambo hilo liliisha juzi pale au lipo mtaani tu, basi ikufikie tu kwamba Yanga hawana jambo dogo ndugu yangu, kama wenyewe wanavyotamba mtaani hawana shughuli ndogo.
Iko hivi leo Juni 4, 2024, baada ya kipindi cha maswali na majibu bungeni, Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson, alimuita Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba kwa ajili ya kuwasilisha bungeni Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Fedha kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025.
Hata hivyo baada ya Waziri Nchemba kusimama na kabla ya kuanza kusoma hotuba yake, alianza kwa pongezi kwa Yanga kutwaa kombe hilo na kumalizia kwa maneno: “Yanga wamejua kutupa raha,” amesema Waziri Nchemba, kauli ambayo ilifuatiwa na makofi ya wabunge kwa sekunde kadhaa.