Raila aagwa Kitaifa kwenye ibada maalum

WAKENYA kutoka maeneo mbalimbali ya nchi hii leo, Ijumaa, wamefurika katika Uwanja wa Michezo wa Nyayo, Jijini Nairobi, kushiriki ibada ya kitaifa ya kumuaga aliyekuwa Waziri Mkuu wa Kenya, Raila Amolo Odinga, aliyeaga dunia akiwa nchini India alipokuwa akipokea matibabu.
Tukio hilo kubwa limevutia maelfu ya wananchi, wakiwemo viongozi wa kisiasa, kidini na wageni wa kimataifa, waliokuja kutoa heshima zao za mwisho kwa mwanasiasa huyo mkongwe ambaye amekuwa kiungo muhimu katika siasa za Kenya kwa zaidi ya miongo minne.
Usalama umeimarishwa ndani na nje ya uwanja huo, ambapo askari wa vikosi mbalimbali wameonekana wakihakikisha utulivu unatawala. Kufikia saa mbili asubuhi, sehemu kubwa ya viti ilikuwa imeshajazwa, huku wafuasi wa Raila wakiimba nyimbo za kumsifu na kuonyesha upendo wao kwa kiongozi waliyeamini kuwa alisimama kwa haki, umoja na demokrasia.
Kulingana na ratiba rasmi iliyotolewa na Serikali, mwili wa marehemu Raila Odinga ulitolewa katika makafani ya Lee mapema alfajiri, kisha kupelekwa kwenye majengo ya Bunge kwa ajili ya wabunge na viongozi mbalimbali kumuaga. Baada ya hapo, mwili wake ulipelekwa moja kwa moja katika Uwanja wa Nyayo kwa ibada ya kitaifa inayoongozwa na viongozi wa dini kuu nchini.
Serikali imetangaza siku ya leo kuwa Siku ya Raila ili kutoa fursa kwa wananchi kumuenzi na kumuaga kiongozi huyo ambaye mchango wake katika historia ya kisiasa ya Kenya unatajwa kuwa mkubwa na wa kipekee.
Naibu Rais, Kithure Kindiki, ambaye anaongoza kamati ya maandalizi ya mazishi, amesema viongozi kadhaa kutoka mataifa jirani na mashirika ya kimataifa wamethibitisha kushiriki katika ibada hiyo. Amewataka wananchi kufika mapema zaidi uwanjani kuanzia saa tatu asubuhi ili kuepuka msongamano na vurugu kama zile zilizoshuhudiwa jana katika Uwanja wa Kimataifa wa Kasarani, ambapo watu watatu walifariki dunia na wengine kadhaa kujeruhiwa wakati wa harakati za kuupokea mwili wa marehemu.
Ibada ya kitaifa inatarajiwa kuendelea hadi alasiri, kisha mwili wa Raila Odinga utasafirishwa kuelekea nyumbani kwake Bondo, Kaunti ya Siaya, ambako mazishi ya kitaifa yatafanyika siku ya Jumatatu.
Raila Odinga, ambaye mara nyingi alitajwa kama “Baba wa Taifa la Pili la Kenya,” amebaki kuwa ishara ya mapambano ya haki, usawa, na demokrasia katika bara la Afrika. SOMA: Kenya : Maelfu Wamuaga Raila Odinga