Rais Museveni kugombea tena urais

UGANDA : RAIS wa Uganda, Yoweri Museveni (80), ametangaza rasmi nia ya kugombea tena urais katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Januari mwaka ujao, hatua itakayomfanya kuongeza muda wake wa utawala ambao umedumu kwa takribani miongo minne.
Kupitia chapisho katika mtandao wa kijamii X (zamani Twitter), Museveni amesema ana matumaini ya kuifikisha Uganda katika uchumi wa dola bilioni 500 ndani ya miaka mitano ijayo, akisisitiza dhamira yake ya kuendeleza maendeleo ya taifa hilo la Afrika Mashariki.
Museveni ametawala Uganda tangu mwaka 1986 baada ya kuingia madarakani kupitia vita vya msituni. Tangu wakati huo, katiba ya nchi hiyo imebadilishwa mara mbili ili kumruhusu kuendelea kugombea nafasi ya urais licha ya vizingiti vya awali vya umri na muda wa mihula.
Hata hivyo, kambi ya upinzani na wanaharakati wa haki za kiraia wameendelea kuushutumu utawala wake wakidai anatumia vikosi vya usalama na rasilimali za serikali kuendeleza uongozi wake na kuwakandamiza wapinzani.
Kiongozi wa upinzani, Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine, naye ametangaza nia ya kugombea urais kwa mara ya pili.
Katika uchaguzi wa mwaka 2021, alishika nafasi ya pili lakini alikataa matokeo, akidai kulikuwa na udanganyifu wa kura, madai ambayo yalikanushwa na Tume ya Uchaguzi na serikali.
Wine ameendelea kuwa mkosoaji mkubwa wa serikali ya Museveni, akieleza kuwa kumekuwa na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu, ikiwa ni pamoja na utekaji nyara, mateso na kuwekwa kizuizini kwa wafuasi na viongozi wa upinzani bila kufuata utaratibu wa kisheria.
Uganda inatarajiwa kufanya uchaguzi wake mkuu wa urais Januari 2026.SOMA: Rais Museveni, Ruto na Hassan wawasili Tanzania