Rais Mwinyi atangaza Baraza Jipya la Mawaziri

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ametangaza Baraza jipya la Mawaziri lenye sura ya mabadiliko na uwiano wa kisiasa, huku akiongeza wizara kutoka 18 hadi 20 ili kuongeza ufanisi wa utendaji wa serikali.
Akizungumza katika hafla iliyofanyika Ikulu Zanzibar leo, Novemba 13, 2025, Dk. Mwinyi amesema baraza jipya limezingatia misingi ya uwajibikaji, kasi ya utekelezaji na matokeo kwa wananchi, akibainisha kuwa katika awamu yake ya pili ya uongozi atakuwa mkali zaidi katika kufuatilia utendaji wa mawaziri wake.
“Tutakuwa wakali katika kufuatilia matokeo. Tunataka ufanisi na tija kwa wananchi. Nimeamua kuongeza wizara mbili ili kuongeza ufanisi wa kazi,” alisema Dk. Mwinyi.
Ametaja wizara mpya kuwa ni Wizara ya Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu, na Wizara ya Vijana, Ajira na Uwezeshaji, ambazo zinalenga kushughulikia changamoto za ajira na kuendana na kasi ya maendeleo ya kidijitali.

Aidha, Rais Mwinyi amesema ameacha wazi nafasi nne za uwaziri kwa Chama cha ACT–Wazalendo, kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar, akieleza kuwa chama hicho kina kipindi cha siku 90 kuamua kama kitaingia au la katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa (GNU). “Nimezitenga nafasi hizi kwa mujibu wa katiba, hadi pale ACT–Wazalendo watakapofanya uamuzi wao,” alisema Rais Mwinyi.
Wizara zilizotengwa ni Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda, Wizara ya Afya, na Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale. SOMA: Mfahamu Waziri Mkuu Mpya

Miongoni mwa walioteuliwa, Dk. Sada Mkuya Salum amekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Ikulu, Dk. Juma Malik Akil ameteuliwa kuwa Waziri wa Fedha na Mipango, huku Idrisa Kitwana Mustafa, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, akiteuliwa kuongoza Wizara ya Tawala za Mikoa na Vikosi Maalum vya SMZ.
Wachambuzi wa siasa wameeleza kuwa uteuzi huo unaashiria mabadiliko ya kizazi katika uongozi wa Zanzibar, kwani sura nyingi mpya na vijana wamepewa nafasi hatua inayotafsiriwa kama mkakati wa Rais Mwinyi kuongeza kasi ya utendaji na kuandaa viongozi wa baadaye.
Rais Mwinyi alihitimisha hotuba yake kwa kusisitiza kuwa serikali yake itaendelea kujikita katika mageuzi ya kidijitali, uwajibikaji na matokeo chanya kwa wananchi. “Nataka kuona jambo la wiki moja linafanyika ndani ya wiki moja, sio miezi mitatu. Wateule wangu wafanye kazi au watupishe,” alisema kwa msisitizo.



