Rais Samia adhamiria kuunganisha Kiswahili, Kihispaniola

RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan ameeleza dhamira yake ya  kuunganisha lugha ya Kiswahili na lugha ya Kihispaniola ambayo ni lugha ya pili kwa kuzungumzwa na watu wengi duniani baada ya lugha ya kiingereza, ili kuwaleta watu wengi pamoja, kuimarisha ushirikiano wa kibiashara, kiuchumi na kiutalii.

Amesema hayo katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo  Dk Damas Ndumbaro wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Kimataifa la Kiswahili katika mji mkuu wa Cuba, Havana.

Advertisement

Ameeleza nia ya kuongeza fursa za ajira kwa vijana kupitia ukalimani kwenye mashirika mbalimbali ya kimataifa na hata kuandaa na kuuza machapisho, huku akisisitiza umuhimu wa wananchi wa Cuba, Ukanda wa Karibe na Amerika ya Kusini  kujifunza kiswahili ili watumie fursa zilizopo Tanzania na Afrika katika shughuli za kiuchumi.

“Tunaamini Kiswahili kitarahisisha na kuwezesha mawasiliano, kwa ajili ya mtangamano, biashara, utalii na uwekezaji barani Afrika kwakuwa  kimekuwa na wazungumzaji wengi na kuwa lugha ya jumuiya mbalimbali za kikanda ikiwemo Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Umoja wa Afrika,”amesisitiza Rais Dk. Samia.

Rais Samia ametoa wito kwa nchi na wadau wa ukanda wa Karibe kuchangamkia fursa ya kujifunza lugha ya Kiswahili ambayo ni lugha ya asili katika bara la Afrika.

Ametumia fursa ya kongamano hilo, kuwaalika wacuba na nchi nyingine za ukanda wa karibe kutembelea Tanzania ili waongee kiswahili na waswahili na kujionea vivutio mbalimbali vya utalii kama vile Mlima Kilimanjaro, mbuga ya wanyama ya Serengeti na visiwa vya Zanzibar ambavyo hali yake ya hewa inafanana na ya ukanda huo ambapo pia ameeleza kuwa Zanzibar ina shule maarufu ya Sekondari iliyopewa jina la Fidel Castrol, kama ishara ya heshima.

Aidha, amefurahishwa na hatua ya kuzindua rasmi Kamusi ya Kiswahili na Kihispaniola ambayo itarahisisha ufunzaji wa lugha na kitabu cha misemo cha Kiswahili na Kihispaniola.