Londo: TBS ni nguzo kuu kulinda afya ya mlaji

DAR ES SALAAM; Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Dennis Londo, amelitaja Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kuwa ni nguzo kuu ya kulinda afya za walaji na kuchochea ustawi wa viwanda nchini.
Amebainisha hayo leo jijini Dar es Salaam katika hafla maalumu ya maadhimisho ya Miaka 50 ya TBS pamoja na utoaji wa tuzo kwa watumishi wa sasa na wastaafu kwa kutambua mchango wao uliojenga misingi imara ya udhibiti wa ubora.
Amesema kutokana na kukua kwa kasi kwa uwekezaji katika sekta za viwanda, kilimo, madini, na nishati, kuna uhitaji wa uwepo mifumo thabiti ya uhakiki ubora, ili kulinda soko la ndani.

Kwa mujibu wa Naibu Waziri huyo, TBS kupitia huduma zake za upimaji na utoaji wa alama za ubora, imekuwa chachu ya kukuza viwanda vya ndani na kuongeza imani ya walaji.
Ameeleza kuwa jambo hil linaiwezesha Tanzania kunufaika kikamilifu na fursa za masoko makubwa ikiwemo Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA).
Amesisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan inaendelea kuweka mazingira wezeshi ya kukuza uchumi kupitia maboresho ya miundombinu ya usafirishaji, nishati, na mifumo ya kidijitali na kwamba maboresho ya sera na sheria yanalenga kuvutia uwekezaji na kuimarisha sekta binafsi.
Ameiasa TBS kuhakikisha kuwa ongezeko la uzalishaji nchini linaenda sambamba na uzingatiaji wa viwango vinavyotambulika duniani.
Akizungumzia mustakabali wa miaka 50 ijayo, Naibu Waziri Londo alieleza kuwa dunia inabadilika kwa kasi kiteknolojia na kiushindani, hivyo kuna mahitaji makubwa ya kuwa na TBS ya kisasa inayoendeshwa kwa maarifa.
Amesema shirika hilo limetakiwa kuwekeza kwenye maabara zenye vifaa vya kisasa zaidi, kuongeza wataalamu wenye ujuzi wa hali ya juu, na kuimarisha mifumo ya kidijitali yenye ufanisi ili kuendana na kasi ya maendeleo ya sayansi na ubunifu duniani.

Mkakati huo wa kuimarisha mifumo ya viwango unaelezwa kuwa msingi imara wa kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayolenga kuifanya Tanzania kuwa nchi yenye uchumi wa kisasa, jumuishi, na unaotegemea uzalishaji wenye thamani kubwa.
Amesema kuwa kusimamiwa vyema kwa usalama na ubora wa bidhaa kutasababisha bidhaa na huduma za kitanzania kukubalika kwa urahisi katika soko la kimataifa na kikanda.

Alitoa rrai kwa sekta binafsi, wazalishaji, na wafanyabiashara kuendelea kushirikiana kwa karibu na TBS ili kujenga utamaduni endelevu wa uzingatiaji viwango na uzalishaji wenye tija.



