RAIS Samia Suluhu Hassan, ametoa Sh milioni 50 kwa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Chamwino Ikulu, kama ahadi ya mchango wake kwenye ujenzi unaoendelea wa kanisa hilo.
Akikabidhi hati ya malipo hayo Jumatatu yaliyofanyika kwa njia ya benki, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule alisema Rais Samia ametoa mchango wake kutimiza ahadi aliyoitoa wakati wa harambee ya ujenzi iliyofanyika Agosti 28, 2022.
“Rais Samia ametoa kiasi hicho kwa kuwa ni kiongozi mwenye hofu ya Mungu, pili kanisa hili ni majirani zake kwani mpo karibu na Ikulu hivyo ametaka kuongeza ujirani wa kiimani. Pia ameweka hazina yake mbinguni kwa Mungu mahali ambapo haitaoza na rais anapenda kuona kila mtu anapata haki ya kuabudu sehemu iliyo salama ili mradi tu haivunji sheria za nchi,” alisema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Gift Msuya alisema harambee iliyofanyika kuchangia ujenzi wa kanisa hilo, imekuwa na mafanikio makubwa kwani ahadi mbalimbali za viongozi zilitolewa na zinatarajiwa kuwasilishwa kwa kanisa mwisho wa Septemba.
Pia ameahidi kushughulikia suala la eneo la wazi ambalo limetolewa na msamaria mwema kwa ajili ya upanuzi wa kanisa lakini kuna sintofahamu zimejitokeza kukwamisha makabidhiano ya eneo hilo.
Akitoa shukrani zake kwa niaba ya kanisa, Askofu wa Kanisa hilo, Amoni Kinyunyu, amemshukuru Rais Samia kwa sadaka aliyoitoa na kumuahidi kwamba wataendelea kufanya kazi kwa bidii kuhakikisha kanisa linakamilika.
Ujenzi wa Kanisa la KKKT Usharika wa Chamwino Ikulu ulianza Aprili mwaka huu baada ya kuona kuna uhitaji wa jengo kubwa kutokana na kuongezeka kwa idadi ya waumini ambapo kwa sasa wapo 400, jengo hilo litakua na uwezo wa kuchukua waumini 600 hadi 800. Ujenzi wake unatarajiwa kugharimu Sh 326,677,500 na linatarajiwa kukamilika Desemba mwaka huu.