Rais Samia amegusa wengi fidia uharibifu wa wanyamapori

AKIWA mkoani Tanga katika ziara yake ya siku saba inayoendelea katika wilaya za mkoa huo, Rais Samia Suluhu Hassan alizungumzia kuhusu changamoto ya wanyama waharibifu wanaoingia katika mashamba ya watu na kusababisha uharibifu.

Akiwa wilayani Lushoto, Rais Samia alisema kutokana na changamoto ya wanyama hao waharibifu, serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kuwalinda wananchi, ikiwamo kuongeza askari wa wanyamapori na kubuni mbinu za kufukuza wanyama, ikiwamo matumizi ya ndege nyuki.

Lakini kwa kuzingatia vilio vya wananchi pamoja na wawakilishi wao wakiwamo wabunge, Rais Samia amemuagiza Waziri wa Maliasili na Utalii kuona uwezekano wa kufanya mapitio ya kanuni za kulipa fidia.

Kwa mujibu wake, wale ambao wanaingiliwa na wanyama kwenye mashamba yao wakaangalie kuhakikisha kweli fidia inayotoka inamlipa mwananchi jasho lake baada ya kuharibiwa mazao na wanyama hao.

Hakuna ubishi kwamba wananchi pamoja na wabunge wao wamekuwa wakipaza sauti kutaka serikali iangalie viwango hivyo vya fidia kutokana na madai ya kupitwa na wakati na pia, kulipwa vikiwa vimechelewa.

Hii inathibitishwa na agizo la Rais Samia ambalo lilitokana na kauli ya Mbunge wa Lushoto, Rashid Shangazi aliyemueleza kiongozi huyo wa nchi kwamba wilaya hiyo inayo changamoto za wanyama waharibifu na serikali iangalie namna ya kuwafidia.

Kwanza, tunampongeza Rais Samia kwa kuiona changamoto hii na kusikia kilio cha wananchi na kuagiza hatua zichukuliwe kurekebisha hali iliyopo.

Ni ukweli maliasili za Tanzania, wakiwamo wanyamapori ni moja ya eneo ambalo limekuwa na mchango mkubwa katika uchumi kupitia utalii na hivyo kusaidia kuongeza Pato la Taifa na kuchangia maendeleo ya wananchi.

Lakini pia katika siku za karibuni, wanyamapori hao katika baadhi ya maeneo wamesababisha uharibifu na maafa, ikiwamo kuvamia mashamba ya wananchi na kuyaharibu kwa kutafuna mazao na pia, kwa baadhi ya wanyama kuua watu.

Kwa kuwa masuala haya ni mtambuka na yanategemeana, ndiyo maana tunaona kwamba agizo la Rais Samia ni jambo jema kwa sababu licha ya kwamba wanyamapori ni maliasili inayotegemewa nchini, lakini inapotokea uharibifu wananchi wanapaswa kufidiwa na wapewe fidia angalau inayoendana na hali halisi ya maisha.

Kwani ni ukweli kuwa fidia zinazolipwa sasa ni ndogo na wakati mwingine zinachelewa, hivyo ni muhimu Waziri wa Maliasili na Utalii na timu yake wakatekeleza agizo la Rais Samia kwa kuja na mapendekezo mazuri ya fidia hizi ili wananchi wanaopata madhara, wasijione wanyonge kwa kifuta jasho kidogo.

Ni muhimu pia, wizara kuendelea kuchukua hatua kama alivyoeleza Rais za kukabiliana na wanyama waharibifu wanaoingia kwenye mashamba na maeneo ya watu na kusababisha madhara, yakiwamo ya vifo.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button