Sh bil 9 kusomesha wataalamu wa afya 601

DAR ES SALAAM:  Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais, Samia Suluhu Hassan umetoa fedha kiasi cha Sh bilioni 9 kwa ajili ya kusomesha wataalam bingwa na bobezi 601 wa fani mbalimbali za afya ili kuongeza idadi ya wataalam wenye ujuzi wa kutoa huduma za kibingwa hapa nchini.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu Novemba 29, 2023 wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mpango wa Rais Samia Suluhu Hassan wa kuongeza wataalam bingwa na bobezi wa afya nchini kwa mwaka wa fedha 2023/24.

“Tunamshukuru Rais, Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kiasi cha Sh bilioni 9 kwa ajili ya mafunzo ya wataalamu bingwa na bobezi katika fani mbalimbali za sekta ya afya ambapo fedha hizo ni muendelelezo wa uwekezaji mkubwa unaofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan.” Amesema Waziri Ummy Mwalimu.

Waziri Ummy amesema fedha hizo zitatumika kugharamia mafunzo kwa wataalamu wapya 601 sawa na 92% ya waombaji ambao walikidhi vigezo vya kusomea utaalamu wa ubingwa na bobezi wa fani mbalimbali za sekta ya afya.

Aidha, Waziri Ummy amewataka wataalamu wote waliopata ufadhili huu wa mwaka 2023/2024 kukamilisha taratibu za kujaza mikataba ya ufadhili kama ishara ya kukubali ufadhili huu.

Amesema kuwa muda wa kujaza mikataba ya ufadhili ni kuanzia Novemba 29, 2023 hadi Disemba 12, 2023 na nakala ya mikataba hiyo inapatikana kwenye tovuti ya Wizara ya Afya na pia itatumwa kwa barua pepe kwenye anuani za barua walizotumia wakati wa kuwasilisha maombi.

Habari Zifananazo

1 Comment
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button