Rais Samia atoa zawadi vituo vya ustawi

RAIS Samia Suluhu Hassan ametoa zawadi ya sukari kilo 2,500 na maji katoni 83 kwa ajili ya sikukuu ya Eid Al-Fitri na Pasaka kwa vituo 24 vinavyotoa huduma za ustawi wa jamii, ikiwemo makao ya watoto kurasini.
Vituo vingine ni mahabusu za watoto, makazi ya wazee na chuo cha watu wenye ulemavu cha Yombo.
Akizungumza Dar es Salaam jana Machi 28,2025 kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan wakati wa hafla ya utoaji wa zawadi hizo, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk Dorothy Gwajima alisema Rais Samia ameendelea kuthibitisha kujali makundi maalum kwa kutoa msaada wa zawadi mbalimbali kwa watoto, wazee na watu wenye ulemavu katika vituo vyote vya ustawi wa jamii.
Amesema katika zawadi hizo zilizotolewa Zanzibar zitapelekwa sukari kilo 500 huku bara zikibaki 2000 pamoja na maji.
“Katika mwaka wa fedha 2024/25, jumla ya Sh milioni 165,317,000 zimetumika kwa ajili ya kutoa zawadi za kuwawezesha watu wenye mahitaji maalum kufurahia sikukuu zijazo na mahitaji hayo yanajumuisha vyakula pamoja na viburudisho,” amesema Dk Dorothy.
Amesema mbali na msaada wa vyakula rais Samia alitoa vifaa mbalimbali kwa lengo la kuwaendeleza watoto na kuimarisha huduma katika makao ya watoto, vikiwemo vifaa vya shule, majiko, mashine za kufulia, majokofu na vitendea kazi vingine huku jumla ya vituo 153 vya Tanzania Bara na Zanzibar vikinufaika na msaada huo.
Mkurungenzi wa Kituo cha yatima cha Amani kilichopo Kigamboni, Hajjaty Zubeida Abdallah amesema zawadi hizo ni faraja kwao kwani kulea na kusimamia vituo hivyo wanaisaidia serikali.
“Tunamshukuru rais Samia kwa kutambua mchango wetu kwani sisi tunapolea haya makundi ni dhahili tunaisaidia serikali kwa kuwapa malezi bora, elimu na mengine ambayo baadae yanasaidia jamii kuleta maendeleo,”amesema Zubeida.
Naye Ofisa Ustawi wa Jamii, Chuo cha Ufundi Stadi na Marekebisho kwa Watu Wenye Ulemavu, Juma Samora ameishukuru serikali kwa kuwakumbuka watu wenye ulemavu kwani inawatia moyo nakuona wanathaminiwa.



