Rais Samia awakumbuka yatima Geita

RAIS Samia Suluhu ametoa zawadi maalum ya sikukuu ya Eid na Pasaka kwa watoto 190 waliopo kwenye vituo vitatu vya kulelea watoto yatima mjini Geita.
Zawadi hiyo inajumuisha chakula na vinywaji vyenye thamani ya sh milioni 13 kwa ajili watoto 144 wa kituo cha Moyo wa Huruma, watoto 18 wa kituo cha Nneemal Wally na watoto 28 wa kituo cha Neema House.
Mkuu wa mkoa wa Geita, Martine Shigella amewasilisha zawadi hiyo kwa niaba ya Rais Dk Samia katika hafla iliyofanyika kituo cha Moyo wa Huruma kilichopo makao makuu ya Jimbo Katoliki la Geita.

Shigella amesema hatua hiyo ni muendelezo wa Rais Dk Samia kuwajali na kuwakumbuka watoto wenye uhitaji hususani kipindi cha sikukuu ili nao waweze kufurahi sawa na watoto wengine walio na wazazi.
Amesema dhamira ya Rais Samia ni kuwafariji watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu, watoto yatima na watoto wenye uhitaji ili kuendelea kuwatia moyo na nguvu ya kusoma na kuzifikia ndoto zao.
Mganga Mkuu wa mkoa wa Geita, Dk Omar Sukari ameainisha zawadi ya Dk Samia ni ndoo 20 za mafuta ya kupikia, sukari mifuko 20, sabuni za unga mifuko 20 na sabuni za vipande boksi 20.

Ameongeza pia kuna katoni 30 za juisi, katoni 30 za maji, mbuzi 14 kwa ajili ya kitoweo, kilo 1,000 za mchele, makopo 20 ya maziwa, unga wa ngano kilo 100 pamoja na unga wa sembe kilo 100.
Msimamizi wa Kituo cha Kulelea watoto cha Moyo wa Huruma, Sister Maria Lauda amesema tangu wameanza kulea watoto wamepiga hatua kubwa kwenye elimu ya msingi, sekondari mpaka chuo kikuu.
“Ninawalika pia wananchi wengine wote kuvijali vituo vya watoto, ili watoto waendelee kufarijika, kufaidika na kuneemeka ili kisaikolojia waendelee kupata uponyaji kwa majeraha waliyonayo”, amesema.
Mwenyekiti wa Kituo cha Kulelea watoto Yatima cha Nneemal Wally, Zaituni Hussein amesema kati watoto 18 wanaowalea, watoto 12 ni kati ya miaka 6-12 huku watoto sita wana umri kati ya 15-16.
Ofisa Ustawi katika kituo cha Neema House, Mussa Erasto aliahidi zawadi ya zilizotolewa zitatumika kwa makusudio ambayo Rais Dk Samia ameyalenga.



