Rais Samia aweka jiwe la msingi barabara Nachingwea

RAIS Samia Suluhu Hassan ameweka Jiwe la Msingi ujenzi wa Barabara ya Nachingwea–Ruangwa – Nanganga sehemu ya Ruangwa- Nanganga (km 53.2) inayojengwa kwa kiwango cha lami leo 18 Septemba 2023.

Akizindua ujenzi wa barabara hiyo Rais Samia amesema serikali imejipanga kujenga miundombinu ya mikoa ya Kusini ili kurahisisha usafirshaji wa mazao na kukuza uchumi wa mikoa hiyo na kuwataka wakandarasi wakamilishe ujenzi wa barabara hiyo kwa wakati.

“Niwaombe wakandarasi na wasimamizi waende kwa kasi sana lakini nipongeze TANROADS mkandarasi na wengine kwa hatua ambayo imeshafikia na kwetu sisi serikali mafedha yapo tunasubiri ‘certificate’ cheti ziletwe tulipe kazi ziendelee.” amesema Rais Samia.

Advertisement

Rais Samia amesema lengo la serikali ni kuunganisha mkoa wote wa Lindi kwa kiwango cha lami na wilaya kwa wilaya ziunganike kwa lami”

“Niwaombe mpokee maendeleo yanayokuja tufanyaje kazi kwa pamoja langu kubwa la kuwaomba maendeleo ni fedha ndugu zangu na fedha inapatikana tunapouza bidhaa na nyinyi ni wakulima wazuri wa ufuta, mbaazi na korosho na bei ya ufuta na mbaazi mmeiona mwaka huu, tunafanya kazi tuone korosho nayo iwe na bei nzuri”- amesisitiza Rais Samia.

Akisoma taarifa fupi ya ujenzi wa barabara hiyo mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mhandisi Mohamed Besta amesema mkandarasi anayejenga barabara hiyo ni China 15th Group kwa thamani ya Sh bilioni 50.3 na jumla ya Sh bilioni 1.1 ikiwa ni sehemu ya ongezeko la thamani na kutumika kulipa fidia ya mali na ardhi kwa watu walioathirika na ujenzi kwa mujibu wa sheria.

“Mheshimiwa Rais ujenzi wa Barabara unasimamiwa na TEKU ambacho ni kitengo cha TANROADS na maendeleo ya ujenzi mpaka sasa tumefikia asilimia 71, na mapaka sasa tumeshalipa jumla ya Sh bilioni 20.7 na zilizobaki tunaendelea kulipa kwa utaratibu uliowekwa.” Amesema Besta.

2 comments

Comments are closed.