Rais Samia na Mapinduzi ya Tanzania ya Kijani kuhifadhi mazingira

KATIKA Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, mazingira yamepewa kipaumbele kama nguzo muhimu ya maendeleo endelevu ya Tanzania. Dira inalenga kuhakikisha taifa linabaki salama dhidi ya majanga yatokanayo na uharibifu wa mazingira kama vile mabadiliko ya tabianchi, ukame, mafuriko, mmomonyoko wa udongo na kupotea kwa bayoanuai.

Kimsingi, Kampeni ya ‘27 ya Kijani’ ya Rais Samia Suluhu Hassan ni mwanzo mzuri wa utekelezaji wa dira hiyo kwa kuibua wananchi, taasisi binafsi na za umma pamoja na wadau wengine wa mazingira nchini kutambua kuwa, mazingira bora ndio msingi wa uhai, afya na maendeleo ya taifa.

Katika muktadha huo, Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limekuwa mstari wa mbele kutekeleza Dira ya Taifa 2050 na kampeni hiyo kwa kuungana na serikali pamoja na taasisi binafsi nchini kupanda miti zaidi ya 5,000 kupitia kanda zake 13 nchini kote.

Baraza hilo linalenga kuhamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika upandaji miti kama hatua ya kukabiliana na changamoto za kimazingira, hususan mabadiliko ya tabianchi. Hatua hiyo inalenga si tu kuongeza uoto wa asili, bali pia kujengea wananchi uelewa na uwajibikaji wa moja kwa moja katika kusimamia na kuhifadhi mazingira yao.

Akizungumza kwa niaba ya mkurugenzi mkuu wa NEMC, Mkurugenzi wa Utawala na Fedha, Dickson Mjinja anasema suala la mazingira ni dhamana ya kimungu na jukumu la kitaifa linalohitaji ushirikiano wa kila mmoja. Anasema jitihada za Rais Samia ni mfano wa kuigwa na zinasaidia kuhamasisha Watanzania kushiriki kwa pamoja kuhifadhi rasilimali za taifa kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Anasema NEMC inaunga mkono jitihada za Rais Samia katika upandaji miti kama hatua muhimu ya kukabiliana na athari mbaya za mabadiliko ya tabianchi, kuongeza rutuba ya udongo na kuboresha ubora wa mazingira na hewa safi pamoja na utekelezaji wa Mkakati wa Maendeleo wa Taifa (NDS). Anafafanua kuwa, upandaji miti unachangia kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDGs) na kukuza uchumi wa kijani kupitia ajira za kijani na matumizi endelevu ya rasilimali asilia kama anavyotekeleza Rais Samia.

Mjinja anasema suala ya kuhifadhi mazingira si jukumu la mtu mmoja au serikali pekee, bali jukumu la kitaifa linalohitaji ushirikiano wa pande zote. Anabainisha kuwa, utunzaji wa mazingira ni suala la kiimani kwa sababu hata kwenye vitabu vya dini inaelezwa kuwa, Mungu aliwapa wanadamu jukumu la kutunza mazingira ikiwemo Bustani ya Edeni. SOMA: Dk Muyungi asihi vijana fursa muungano, mazingira

Baada ya kumaliza kupanda miti katika Zahanati ya Vingunguti (Dar es Salaam), Mjinja anasema wamepanda miti hiyo kuunga mkono juhudi za Rais Samia katika kukuza na kutunza mazingira. Anasema miti hiyo itakuwa sehemu ya kumbukizi ya kudumu kwa sababu wana imani uongozi uliopo utaitunza ipasavyo. “Tuna imani miti hii itatunzwa vizuri, tunaomba kila mtu atambue kuwa uhifadhi ni jambo muhimu na bora katika utunzaji wa mazingira yetu kwa sababu miti ni uhai,” anasema.

Anaongeza: “Katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, inasaidia kuifanya Tanzania kuwa na hali nzuri ya hewa ambayo itatusaidia kukabiliana na mabadiliko hayo.” Anatoa wito kwa wananchi wote kila mmoja kwa nafasi yake kujitahidi kupanda miti na kuzingatia uhifadhi wake, kwa kuzuia ukataji holela wa miti ili kufanikisha lengo la Rais Samia la kuwa na Tanzania ya kijani.

Aidha, NEMC inasema itaendelea kuhimiza na kuunga mkono juhudi za upandaji miti kama mkakati wa msingi wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Kwa mujibu wa NEMC, upandaji miti huchangia kwa kiasi kikubwa katika kufyonza gesijoto, kuhifadhi vyanzo vya maji, kulinda bayoanuai na kuimarisha ustahimilivu wa jamii dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi.

Anasema NEMC pia inatambua upandaji miti kama nguzo muhimu ya ajenda ya uchumi wa kijani inayolenga kukuza uchumi unaozalisha ajira za kijani na kuongeza kipato cha wananchi sambamba na kuhakikisha matumizi endelevu ya rasilimali asilia bila kuhatarisha mustakabali wa vizazi vijavyo.

Kwa kuunga mkono mfano wa uongozi wa bora wa Rais Samia, NEMC inasema itaendelea kusimamia, kuratibu na kuhamasisha utekelezaji wa shughuli za uhifadhi wa mazingira ili kuhakikisha Tanzania inatimiza ahadi zake za kitaifa na kimataifa katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kufikia maendeleo endelevu.

Meneja wa Tafiti za Mazingira wa NEMC, Dk Rose Sallema anasema ukataji haramu wa miti umeleta na kusababisha athari kubwa duniani likiwemo ongezeko la athari za mabadiliko ya tabianchi, kupotea kwa makazi ya wanyamapori na mmomonyoko wa udongo unaochangia kupungua kwa mazao ya kilimo.

“Kwenye miti tunapata vitu vingi, kwa hiyo tukipanda miti tunatengeneza mazingira ya kuwa na viumbe hai wa aina mbalimbali lakini pia tunatengeneza mazingira ya kuhifadhi maisha yetu,” anasema. Dk Sallema anaongeza: “Tunashuhudia kabisa ukataji wa miti unavyosababisha matatizo mengi duniani, ikiwemo kuondoa viumbe hai na mabadiliko ya tabianchi.” Anasema

NEMC itaendelea kushirikiana na wadau wa utunzaji wa mazingira katika kupanda miti na uhifadhi wa mazingira ili kuwezesha Tanzania kuepuka majanga yatokanayo na kutokutunza mazingira na hivyo, kuharakisha maendeleo endelevu ya taifa. Mkazi wa Dar es salaam, Zena Saleh anasema anatambua ukweli kuwa kupanda miti ni kila kitu katika maisha ya binadamu.

Anatoa wito kwa vijana na wananchi kwa ujumla kuwa na utamaduni wa kupanda miti ili kujikinga dhidi ya athari za ukataji miti. Anasema kipindi cha nyuma, miti ilikuwa inakatwa lakini si kama inavyokatwa sasa kwa sababu watu walikuwa wakitumia mbolea ya miti katika mashamba na mazingira hayakuathirika, kwa kuwa walikuwa wakipanda mingine.

Anasema kwa sasa hali ni tofauti, kwani miti imeathirika zaidi ndio maana kuna ukosefu wa mvua za kutosha na hali ya hewa yenye athari zisizotabirika wala kufahamika kwa uhakika. Hivi karibuni, Mkurugenzi Msaidizi (Sehemu ya Hifadhi ya Bayoanuai) Idara ya Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Dk Deogratius Paul alisema kupitia kampeni ya upandaji miti chini ya Rais Samia, Tanzania imepanda na kustawisha miti 691,523,763 katika kipindi cha miaka minne kuanzia mwaka 2020-2024.

Januari 27, 2026 Rais Samia aliadhimisha kumbukizi ya siku ya kuzaliwa kwake kwa kupanda miti katika maeneo ya Bungi Kilimo na Kizimkazi, Zanzibar chini ya Kaulimbiu: “Uzalendo ni Kutunza Mazingira”, Shiriki Kupanda Miti.

Habari Zifananazo

2 Comments

  1. Howdy! This is my first visit to your blog! We are a collection of volunteers and starting a new project in a community in the same niche.
    Your blog provided us useful information to work on. You have done a wonderful job!

  2. My best friend’s sister gets $180 an hour on the internet… she’s been laid off for two months, the previous month her paycheck was $20328 only working at home for a couple of hours each day…

    check out……… http://www.jobathome1.com

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button