Rais wa Namibia atoa somo la uongozi

RAIS wa Namibia, Netumbo Nandi-Ndaitwah amesema nidhamu na kuwa na malengo ni msingi wa kuwa kiongozi mzuri.
Alisema hayo alipozungumza katika mhadhara wa kitaaluma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) jana.
Alisema kwa kuzingatia mfano wake, alipotoka Rais Samia Suluhu Hassan na wengine waliofikia nafasi walizonazo ni wazi malengo na nidhamu ndiyo miongozo mikuu iliyowafikisha walipo leo.
“Mimi na Rais Samia tumewahi kuwa mawaziri wa mazingira na utalii katika nchi zetu kwa wakati mmoja, hatukuwa karibu sana lakini kwa kuwa Tanzania na Namibia zimekuwa karibu tumekuwa tukikutana bila kujua kwamba siku moja tutakuwa kwenye nafasi tulizonazo sasa. Ni wazi kwamba kuwa na malengo na nidhamu ndio msingi wa haya,” alisema.
Rais Netumbo alisema si kila mmoja atakuwa rais lakini kila mmoja ana hatma yake na ili kuifikia anahitaji kuijenga kuanzia mapema kwa namna anavyojiongoza na anavyowaongoza wengine.
Alisema katika kila hatua ya kufikia alipo amejifunza kujitoa na kujua alichokitaka kumemsaidia kufikia malengo na kwamba katika kutimiza hilo watakuwepo watakaosema maneno mengi na ya kukatisha tamaa lakini kubaki kwenye malengo ni suluhu.
Rais Netumbo alisema yeye hakuchaguliwa kwa kuwa ni mwanamke ila aliweza kuwathibitishia Wanamibia yupo tayari na ana uwezo wa kuwatumikia.

“Kwa wanawake, unapokuwa kwenye nafasi fulani kuwa wewe, kwa sababu kutakuwa na changamoto zinazoweza kukutoa kwenye mstari usipokuwa imara na hazitakuja kutoka kwa wanaume pekee bali kwa jamii nzima. Unachotakiwa kufanya ni kubaki kwenye maamuzi na kutimiza malengo yako,” alisema.
Rais Netumbo alisema tofauti na zamani, wanawake kwa sasa wana bahati ya kupata elimu bora na katika mazingira mazuri hivyo ni jukumu lao kuitumia ipasavyo kufanya mambo ya kuacha alama.
“Wanawake wana uwezo sawa pamoja na maarifa yanayowawezesha kujenga nchi, bara na dunia kwa ujumla kwa kuhakikisha kwamba wanafanya hivyo kwa kuweka nguvu ya kutosha,” alisema.
Rais Netumbo alisema alianza siasa akiwa mdogo na hilo limemsaidia kwa kuwa ameona vitu vingi ambavyo vilimuweka katika nyakati ngumu alizoweza kuzishinda na kumuimarisha na kuaminiwa kuongoza tangu wakati huo hadi sasa.
Alisema wazazi wake walimweleza akiwa mdogo alikuwa mkimya na alipenda kujiweka karibu na waliokuwa na umri mdogo zaidi yake pamoja na waliokuwa na shida jambo ambalo limemjenga kuwa alipo leo.
Netumbo alisema kuna mambo aliyoyafanya kuleta mageuzi katika utendaji wa kijamii ikiwa ni pamoja na kubadili uamuzi wa Baraza la Mawaziri kuhusu uwezekano wa mwanamke kuruhusiwa kuihudumia familia anapokuwa na uwezo kumzidi mume.
Alisema aliandika barua kwa kueleza tafsiri halisi ya kichwa cha familia kwamba kwa kuwa yeye ndiye aliyekuwa na kipato zaidi alitakiwa kumhudumia mumewe ndipo ukatoka uamuzi kwamba mwenye mshahara mkubwa ndiye atahudumia familia.



