Rasmi Novemba 17 Siku ya Watoto Njiti Duniani

DAR ES SALAAM: SHIRIKA la Afya Duniani (WHO) limetangaza rasmi kuijumuisha Novemba 17 katika kalenda yake ya kimataifa kama Siku ya Watoto Njiti Duniani.

Hatua hiyo ya kihistoria ni katika kutambua na kuimarisha juhudi za kimataifa za kulinda maisha ya watoto wanaozaliwa kabla ya kufikia muda kamili wa ujauzito.

Tangazo hilo limepokelewa kwa shangwe duniani kote, hasa katika nchi zinazoendelea kama Tanzania, ambayo imetambuliwa kuwa miongoni mwa vinara wa juhudi za kuboresha huduma kwa watoto wachanga hususani watoto njiti.

Katika taarifa rasmi, Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dk  Tedros Adhanom Ghebreyesus, imeeleza kuwa uwepo wa siku maalum ya kimataifa kwa watoto njiti utasaidia kuongeza uelewa wa jamii kuhusu changamoto zinazowakumba watoto hao, kuimarisha sera za afya za mama na mtoto, na kuvutia uwekezaji wa kimataifa kwenye huduma za watoto wachanga.

“Ninampa pongezi nyingi Doris Mollel kwa kazi yake kubwa ya kuhamasisha na kuelimisha jamii kuhusu watoto wanaozaliwa kabla ya wakati. WHO itaendelea kuunga mkono juhudi hizi za kuokoa maisha ya watoto wachanga duniani,” ameandika Dkt. Tedros kupitia ukurasa wake wa X (zamani Twitter).

Tanzania imepata heshima kubwa kupitia juhudi za Doris Mollel, mwanzilishi wa Doris Mollel Foundation (DMF), ambaye alizaliwa njiti na kugeuza simulizi yake kuwa chombo cha mabadiliko ya kijamii.

Kwa zaidi ya miaka saba, taasisi yake imekuwa mstari wa mbele katika kutoa elimu kwa jamii kuhusu watoto njiti, kuchangisha na kusambaza vifaa tiba katika zaidi ya hospitali 20 nchini, na kutoa mafunzo ya kitaalamu kwa wahudumu wa afya wanaohudumia watoto wachanga.

Samia katika maadhimisho siku ya wanawake kitaifa

Akizungumzia tangazo hilo la WHO, Doris Mollel amesema: “Kupitishwa kwa Novemba 17 na WHO kuwa siku ya mtoto njiti ni heshima kubwa kwa watoto njiti duniani. Kwa upande wangu na kwa Tanzania, hii ni zawadi ya juhudi za miaka mingi. Dunia sasa itasikia kilio cha watoto hawa na kuchukua hatua madhubuti,” amesema

Aidha, Doris ametoa shukrani kwa viongozi waliounga mkono jitihada hizo akiwemo Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Tedros, Ubalozi wa Tanzania Geneva, na Balozi Hoyce Temu kwa msaada na ushawishi wa kidiplomasia.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button