RC Dar aifagilia Puma Energy kuhusu nishati safi

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesema uamuzi wa Kampuni ya Puma Energy Tanzania kutoa mitungi 1,000 ya gesi katika mkoa huo kuwapatia mama lishe na baba lishe unakwenda kuchochea kasi ya kuzuia matumizi ya nishati chafu ya kuni na mkaa.
Akizungumza leo Oktoba 11, katika viwanja vya Biafra Kinondoni, Dar es Salaam alikopokea mitungi hiyo iliyotolewa na kampuni hiyo, Chalamila amesema uamuzi huo umekuja wakati sahihi kwani dhamira ya serikali ni kutumia nishati safi ya kupikia.

Chalamila amesema Dar es Salaam ni kinara wa matumizi ya nishati chafu, hivyo uamuzi wa kugawa mitungi hiyo itasaidia kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia na kusisitiza kuwa kupika kwa gesi ni nafuu ukilinganisha na kuni au mkaa.
SOMA: Tumuunge mkono Rais, matumizi ya Nishati Safi
“Dar es salaam ndio mkoa unaotumia nishati chafu kutokana na wingi wa watu wanaotumia kuni na mkaa kwa ajili ya kupika hivyo uamuzi huu wa Puma Energy Tanzania unakwenda kumaliza au kupunguza matumizi ya nishati chafu katika mkoa wetu na Tanzania kwa ujumla.

Akigusia faida za kutumia nishati safi amesema ni pamoja na kusaidia kuokoa muda mwingi unaotumika kupika kwa kuni na mkaa, kuokoa gharama na kubwa zaidi ni kuepuka madhara ya kiafya yanayosababishwa na matumizi ya kuni na mkaa.
Mkurugenzi Mkuu wa Puma Energy Tanzania, Fatma Abdallah amesema kampuni hiyo imedhamiria kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan katika kampeni ya matumizi ya nishati safi ya kupikia na ndio wameitoa mitungi hiyo ambayo itagawanywa katika wilaya zote tanı za mkoa huo.

“Katika Mkoa wa Dar es Salaam kuna shughuli nyingi miongoni mwa shughuli hizo ni biashara ya chakula kinachoandaliwa kwa wingi kutoka kwa mama lishe ambao wanakumbana na changamoto nyingi, mojawapo ikiwa upatikanaji wa nishati ya kupikia, hususan nishati safi na salama,” ameeleza.




