KATAVI: NAIBU Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais, Christina Mndeme ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Katavi kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan juu ya kuhamasisha matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia.
Mndeme katika kuunga juhudu hizo ameanza ziara mikoa ya Nyanda za Juu Kusini mwa Tanzania kwa ajili ya kutoa elimu na kuhamasisha matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia ambapo Septemba 17 alikuwa mkoani Katavi.
Amesema lengo ni kutoa elimu hiyo mikoa yote Tanzania ambapo kwa sasa mikoa itakayonufaika na elimu ya Nishati Safi ya Kupikia ni pamoja na Rukwa, Songwe, Mbeya na Njombe.

Ameongeza kuwa katika kuhakikisha kila mtanzania anatumia nishati safi ya kupikia Serikali inafanya juhudi mbalimbali ikiwemo kukaribisha wawekezaji ambapo mtumiajia atakuwa na uhuru wa kutumia gesi kulingana na kiwango cha fedha anachokihitaji kama ilivyo kwenye luku.
“Nimefurahi kuona hapa Mpanda hampo nyuma katika matumizi ya Nishati Safi kulingana na maelezo mbalimbali yaliyotolewa na uongozi hapa na hii ndicho tunachokihitahi hadi mwaka 2034 zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania wawe wanatumia Nishati Safi.
“Hii inaonyesha namna gani watu wa Mpanda mnavyomuunga mkoa Rais Samia yeye akiwa ‘champion’ namba moja wa Nishati Safi ya Kupikia ndio maana leo tumekutana hapa ili tuongee na kuona umuhimu wa kutumia nishati hii,” amesema Mndeme.

Kwa upande wake, Naibu katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Felista Mdemu amesema nishati imekuwa kikwazo cha maendeleo tangu miaka ya nyuma lakini jukumu tulilonalo ni kuchagua nishati iliyo salama juu ya maisha yetu.
“Ikumbukwe agenda hii ni ya Rais wetu ambaye ni kinara wa matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia hivyo uwepo wetu hapo ni katika jitihada za kuhakikisha agenda hii inafanikiwa.
Hata hivyo Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Katavi, Nehemia James amesema katika kuunga matumizi ya Nishati Safi mkoa umekuwa ukigawa mitungi ya gesi kwa watu wa makundi mbalimbali hasa ya kina mama.
“Wakati wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2024 tumegawa mitungi ya gesi na mpango wetu kama mkoa kila wiki ya ‘Mwana Katavi’ ambayo huadhimishwa kila mwaka na kwa mwaka huu tutafanya kongamano na kugawa mitungi ya gesi,” amesema James.