Fursa ‘zanukia’ maandalizi mnada vitalu vya gesi yakikamilika

LONDON, UINGEREZA: Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), Mhandisi Charles Sangweni amesema maandalizi muhimu kuelekea mnada wa vitalu vilivyo wazi vya utafutaji wa gesi asilia yamekamilika huku akiwataka wadau kuwa tayari kuchangamkia fursa mbalimbali kwenye sekta hiyo muhimu ya nishati.

Mhandisi Sangweni amebainisha hayo katika mkutano ulioangazia masuala ya nishati Afrika uliofanyika jijini London, Uingereza leo (Mei 14, 2026) wakati akiwasilisha mada kuhusu fursa za uwekezaji katika sekta ya mafuta na gesi asilia nchini kwenye Kongamano la Nishati Afrika.

“Kinachosubiriwa kwa sasa ni kuidhinishwa kwa Mkataba Kifani wa Uzalishaji na Ugawanaji Mapato wa Mafuta na Gesi Asilia (Model Production Sharing Agreement – MPSA). Mara baada ya kuidhinishwa kwa MPSA hiyo, mchakato wa mnada wa vitalu utaanza mara moja,” alisema Sangweni katika mkutano huo uliohudhuriwa na wadau kutoka sehemu mbalimbali duniani.

Mkuu huyo wa PURA alibainisha kuwa sekta ya mafuta na gesi asilia nchini Tanzania ina fursa kubwa na zenye mvuto kwa uwekezaji huku akiwahimiza kuwahimiza wadau mbalimbali wa sekta hiyo kuchangamkia fursa zilizopo.

SOMA: Chevron: Tupo tayari kuwekeza Tanzania 

Alieleza kuwa taarifa (data) mbalimbali za vitalu vilivyo wazi zinapatikana kwa ajili ya wawekezaji kuziona na kuzinunua kwa madhumuni ya tathmini na uwekezaji.

Baadhi ya taarifa hizo, kwa mujibu wa Mhandisi Sangweni ni pamoja na zile zinazohusu nguvu sumaku ya miamba (magnetic forces), uzito wa miamba (gravity), mitetemo ya 2D na 3D pamoja na taarifa za visima.

Wadau wa sekta ya nishati walifuatilia wasilisho la Mkurugenzi Mkuu wa PURA, Mhandisi Sangweni jijini London

Mbali na hilo, Mhandisi Sangweni alisema kuwa ipo fursa kwa wawekezaji kushirikiana na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) katika kuendeleza vitalu vya Lindi–Mtwara, Eyasi-Wembere, Mnazi Bay Kaskazini na Songo Songo Magharibi ambavyo TPDC imeendelea kuvifanyia shughuli za utafiti wa mafuta na gesi asilia.

Aliongeza kuwa utekelezaji unaoendelea wa miradi mbalimbali katika mkondo wa juu wa petroli, ikiwemo mradi wa uchimbaji wa visima vya uzalishaji wa gesi asilia katika Kitalu cha Mnazi Bay mkoani Mtwara umeendelea kuongeza imani kwa wawekezaji na wadau wa sekta hiyo kuwekeza nchini Tanzania.

“Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini, jambo ambalo limeendelea kuongeza imani kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuwekeza Tanzania katika sekta mbalimbali, ikiwemo sekta ya mafuta na gesi asilia,” alisema Sangweni.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button