RC Geita aonya migogoro watumishi wa umma
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shigella amewataka watumishi wa umma kuacha kuvutana wawapo ofisini badala yake waungane kusimamia maadili na wajibu ya utumishi kwani ndio muhimili wa serikali.
Shigella amesema hayo alipokuwa akizungumuza na watumishi wa umma wa halmashauri zote mkoani Geita katika ufunguzi wa semina ya Sekreteriati ya Maadili ya viongozi wa umma kanda ya ziwa.
Amesema maadili ya viongozi ndio msingi wa mafanikio kwa taifa lolote inayoshadadia maendelea na usawa kwa taifa na kuwafanya watanzania waweze kunufaika na taifa lao kupitia serikali yao.
“Tukiyazingatia haya yote taifa letu tutaendelea kuwa amani, tutaendelea kuwa na umoja, tutaendelea kuwa na mshikamano na wananchi wataishi kwa kupendana.
“Chuki kati ya mwenye nacho na asiye nacho, chuki kati ya mwenye madaraka na asiye na madaraka, haina nafasi kama mmejenga misingi yenye uwazi na uwajibikaji.” Amesema
Katibu Msaidizi Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kanda ya Ziwa, Godson Kweka amesema utaratibu wa kutoa mafunzo kwa watumishi unalenga kukumbusha haki na wajibu kwa watumishi.
“Tunasisistiza viongozi wawe wanatunza siri, lazima kiongozi awe na uwezo wa kutunza siri, kwa hiyo tunawaelekeza, tunawaelimisha, umuhimu wa kutunza siri za serikali.” Alieleza Kweka.
Amesema msisitizo mkubwa ni sheria ya maadili ya viongozi wa umma, miiko ya uongozi, uwajibikaji wa pamoja na kuepuka mgongano wa maslahi kwa kuwa hakuna maendeleo pasipo kuwa na maelewano.
“Kiongozi hatakiwi kutumia nafasi yake kujinufaisha yeye mwenyewe, anatakiwa atumie hiyo nafasi kwa ajili ya manufaa ya umma, maamuzi yote anayofanya yawe yanalenga kwa maslahi ya umma.”
Akifunga semina hiyo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita, Prof Godius Kahyarara amewataka viongozi wote kuheshimu mipaka ya kila mmoja na kupeana nafasi ya kushauriana kwa maendeleo ya mkoa.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Geita, Zahra Michuzi amekiri mafunzo ya sekreteriati ya maadili kwa viongozi hasa waajiriwa na wateule wapya na kuwaongezea uwezo wa kutumikia ofisi za umma.