RC Geita awatimua maofisa wa GGML kikao cha RCC

MKUU wa Mkoa wa Geita, Martine Shigela ameamuru maofisa watendaji watatu wa Kampuni ya Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGML) kutoka nje ya ukumbi wa kikao cha Kamisheni ya Ushauri ya Mkoa (RCC).

Uamuzi wa Shigela unakuja kufuatia kutoridhishwa na majibu ya maofisa hao wa GGML juu ya malipo ya malimbikizo ya fedha za Uwajibikaji wa Makampuni kwa Jamii (CSR) mwaka 2024 sh bilioni tisa.

Shigela amechukua hatua hiyo na akieleza kuwa fedha za CSR ni fedha za wananchi na siyo mtumishi wa GGML na hazitolewi kama hisani bali ipo kwa mujibu wa sheria na GGML haipaswi kuleta mzaha.

“Sasa nyie mmejitengenezea kanuni za wapi? kwamba hiyo CSR ya mwaka jana imefutwa, na je serikali ndio imechelewesha mpango kazi au nyie ndio mmechelewesha.

“Msilete mchezo, hakuna biashara ya ujanja ujanja kama hiyo, bilioni tisa za wananchi za maendeleo mnataka kuichukua hivi hivi, na nyie mnaamini kabisa Geita Gold Mining mpo sahihi.

“Yaani kweli menejimenti yote ya GGML mmekaa mmeamua mfanye hivo, tokeni nje mkaendelee na kazi yenu, siku mkizirudisha ndio mtakuja hapa, mnataka kuleta upuuzi hapa,” amesema Shigela.

Shigela amewapiga marufuku maofisa wote wa GGML kufika ofisini kwake mpaka pale ambapo watakuwa wametoa mrejesho sahihi wa fedha ya CSR ya mwaka 2024.

“Mpaka mtuletee fedha ndio mtakuja, kama hamleti fedha msije kabisa ofisini kwangu, mtaenda TAMISEMI au mtaenda madini,” amesisitiza Shigella.

Mbunge wa Jimbo la Chato, Dk Medard Kalemani amepongeza hatua ya Mkuu wa Mkoa kwa kuchukua uamuzi huo kwani CSR ipo kwa mujibu wa sheria ya madini na hivvo GGML wanapaswa kuomba radhi.

“Kwa mujibu wa sheria ya madini, kifungu cha 105, na kwa mujibu wa kanuni ya CSR ya 2023, CSR inapaswa kulipwa kila mwaka, hii ni kwa mujibu wa sheria,” amesisitiza Dk Kalemani.

Mbunge wa Jimbo la Geita Mjini, Costantine Kanyasu amesema GGML hawapaswi kunyenyekewa kwa kile wanachokitoa kama CSR kwani ni kiwango cha kawaida ambacho kinaendana na matakwa ya sheria.

Awali Mwanasheria Mkuu wa GGML, David Nzaligo amefafanua kuwa kampuni ilitenga fedha kwa ajili ya CSR 2024 lakini halmashauri hazikuwasilisha mpango kazi kwa wakati na kufanya fedha kuondolewa kwenye mpango.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button