MKUU wa Mkoa wa Kagera, Fatuma Mwasa ameiomba Wizara ya Kilimo kujenga masoko ya zao la ndizi mpakani ili kuwainua wakulima kiuchumi.
Akizungumza leo Oktoba 16, katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani, RC Mwasa amesema licha ya mkoa huo kuwa na mchango mkubwa katika kuzalisha ndizi bado mkulima anapata manufaa kidogo ukilinganisha na wakulima wa mazao mengine.
Amesema masoko ya mpakani yatawasaidia wakulima kupanua wigo na masoko ya nje ikiwemo kufika moja kwa moja kwani wafanyabiashara wanaoenda kununua mashambani wanashusha thamani ya ndizi zaidi.
“Mkungu mmoja wa ndizi kilogramu 50 wanaouza mkulima wa Bukoba ,Karagwe, Kyerwa na Muleba ni Sh 3,000 hadi 10,000 hii sio sawa, tuna wafanyabiashara wengi wanaotoka katika mataifa jirani kuja kununua ndizi lakini hawawezi kukutana na mkulima tunaamini kupitia mipaka yetu mingi kama tutakuwa na soko la ndizi la kudumu wakulima watanufaika na bei ya zao lao,” amesema RC Mwasa.
Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde amesema ujenzi wa soko la ndizi katika wilaya zinazozalisha ndizi kwa wingi Kagera serikali italifanyia kazi haraka iwezekanavyo.
Amesema kwa sasa wananchi wa Tanzania hawana uhitaji wa chakula kwani taifa limezalizalisha chakula kwa asilimia 128.
Amesema miaka mitatu nyuma, bajeti ya kilimo ilikuwa Sh bilioni 225 na sasa bajeti hiyo imepanda hadi kufikia tril 1.2 jambo linalopelekea kuimarika kwa Kilimo uzalishaji na uuzaji wa chakula nje ya nchi.
View this post on Instagram