RC Kigoma ageukia wazazi utoro wa wanafunzi

KIGOMA; Mkuu wa Mkoa Kigoma Balozi Simon Sirro, amewataka walimu wakuu wa shule za msingi, kamati za shule na ofisi za watendaji wa mitaa na kata kuwachukulia hatua za kisheria wazazi ambao wamekuwa kichocheo cha utoro sugu kwa watoto wao.
Balozi Sirro alisema hayo akifanya ziara katika baadhi ya shule za msingi za Manispaa ya Kigoma Ujiji, baada ya matokeo ya mtihani wa darasa la saba, ambapo alisema kuwa baadhi ya wazazi wamekuwa kichocheo kikubwa kwa watoto wao kushindwa kuhudhuria masomo.
Amesema kuwa sheria ya elimu inafafanua namna shule na kamati za shule zinavyoweza kuchukua hatua kwa wazazi wazembe wanaoshindwa kusimamia elimu ya watoto wao, ikiwemo kwa watoto wasiohudhuria masomo hivyo lazima sheria hiyo ifanye kazi kwa wazazi wazembe.

Amewapongeza walimu wa shule za msingi mkoa Kigoma kwa kuwezesha mkoa huo kufanya vizuri kwenye mitihani ya darasa la saba, akieleza kuwa serikali inaendelea kuzifanyia kazi changamoto zinazojitokeza ikiwemo uhaba wa walimu, vitendea kazi na motisha kwa walimu.
Akiwa katika shule ya Msingi Bushabani, Mwalim Mkuu wa shule hiyo, Ramadhan Thabiti alisema kuwa shule hiyo kwa sasa ina wanafunzi wengi ikiwa na wanafunzi zaidi ya 2000 shule ikikabiliwa na idadi kubwa ya utoro kwa wanafunzi na walipofuatilia waligundua wanafunzi wengi wanalelewa na mzazi mmoja au kulelewa na bibi wakati wazazi wakiishi maeneo mengine.




