RC Kigoma azibana halmashauri hoja za CAG

KIGOMA; MKUU wa Mkoa Kigoma, Thobias Andengenye, ametoa siku 30 kwa  halmashauri zote za Mkoa Kigoma kuhakikisha zinazifanyia kazi na kuzifunga hoja zote za ukaguzi zilizoibuliwa na ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Andengenye amesema hayo akizungumza na madiwani na wakuu wa idara za Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza, wakati wa baraza maalum la kuwasilisha hoja za CAG, ambapo aliagiza kuwa hadi kufikia Julai 30 hoja 29  za mwaka wa fedha 2021/2022 na hoja 24 za mwaka wa fedha 2022/2023 za halmaahauri hiyo ziwe zimefungwa.

Amesema kuwa agizo lake linakuja kukiwa na hoja za ukaguzi ambazo zimekuwa zikijirudia kila mwaka, ukaguzi kwa halmashauri zote za mkoa huo unapofanyika na hasa kuhusu matumizi yasiyozingatia sheria, kanuni na taratibu za fedha, pamoja na watumishi kushindwa kutumia taaluma zao katika kushughulikia masuala ya fedha na usimamizi wa majukumu yaliyo chini yao.

Kwa upande wake mwakilishi wa Mkuu wa Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali Mkoa Kigoma, Nelson Rwezaura amesema kuwa sababu kubwa ya kuzaliwa kwa hoja kunatokana na idara zote kutofanya kazi kwa ushirikiano na watendaji wengi wanadhani ukaguzi huo unahusu idara ya fedha bila kutilia maanani kwamba, idara zinazofanya matumizi zina wajibu wa kufuata sheria na taratibu za fedha.

SOMA: Chalamila: Msikimbie hoja za CAG

Akiwasilisha hoja hizo za CAG kwenye kikao hicho, Mkaguzi wa ndani wa Halmashauri ya Wilaya Uvinza, Benedict Kiranda amesema kuwa jumla ya hoja 24 zimeibuliwa kwenye  mwaka wa fedha 2022/2023, huku sehemu kubwa ya hoja hizo zikiangukia katika upungufu wa nyaraka na maelezo yasiyojitosheleza ya matumizi ya fedha na utekelezaji wa shughuli zilizopangwa.

Akifunga kikao hicho Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Uvinza, Jackson Mateso amesema wamepokea maelekezo na maagizo yaliyotolewa na kwamba watayafanyia kazi kuhakikisha hoja zinafungwa, lakini wanaweka mikakati ya kuhakikisha halmashauri haizalishi hoja mpya.

Habari Zifananazo

Back to top button