RC Moro ataka habari za uchunguzi migogoro ya ardhi

MKUU wa Mkoa wa Morogoro, Fatma Mwassa ametoa wito kwa waandishi wa habari wa mkoa huo kuandika habari za uchunguzi zitakazosaidia kuzipatia ufumbuzi changamoto za migogoro ya ardhi inayosababisha kutokea kwa mapigano baina ya wafugaji na wakulima.
Mwassa ametoa rai hiyo Desemba 30, 2022 mjini Morogoro katika hotuba yake ya ufunguzi wa mkutano mkuu wa mwaka wa wanachama wa Klabu ya waandishi wa habari Mkoa wa Morogoro.
Amesema waandishi wa habari wana nafasi kubwa ya kuhakikisha wanaandika kwa kina habari zitakazoleta suluhu ya kwenye migogoro ya wakulima na wafugaji, ambayo imekuwa ikijitokeza mara kwa mara mkoani Morogoro.
Mwassa amesema njia pekee ya kutafutia suluhu ya changamoto hiyo ni kuwa na mkakati wa pamoja utakahusisha wadau mbalimbali, wakiwemo waandishi wa habari ambao kutokana na taaluma waliyokuwa nayo itasaidia kuwaelimisha na kuwahamasisha wananchi kuepuka matumizi ya ardhi kiholela na kuzingatia sheria badala ya kurubuniwa na madalali wanaotoa hati feki.
Amesema mbali na changamoto za migogoro ya ardhi, pia wapo baadhi ya watu wanaovamia maeneo ya hifadhi ukiwemo msitu wa kuni uliopo eneo la Kiegea mpakani mwa wilayani Mvomero na halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Mwassa amesema mkoa huo pia una changamoto ya matukio ya ukatili wa kijinsia, huku akilitaka Jeshi la Polisi mkoa huo kuongeza kasi ya ufuatiliaji wa matukio ya ukatili wa kijinsia na utoaji wa taarifa za matukio hayo kwa wakati, ili watuhumiwa wafikishwe kwenye vyombo vya sheria.
Katika hatua nyingine amesema Ofisi yake inaandaa mpango mkakati maalum unaotarajia kutoa tuzo kwa waandishi wa habari watakaojikita katika kufanya utafiti juu ya utatuzi wa migogoro ya ardhi, migogoro ya wakulima na wafugaji na jinsi ya kukabiliana na ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto.
Mwassa amesema tuzo hizo za umahiri atazianzisha na zitatolewa kwa kushindanisha kazi ambazo zitafanywa na waandishi wa habari.
Naye Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Morogoro, Nickson Mkilanya amesema waandishi wa habari Mkoa wa Morogoro watamuunga mkono Mkuu huyo wa mkoa katika ajenda ya serikali ya kupambana na migogoro ya ardhi,matumizi holela ya rasiliamali ardhi yanayosababisha uwepo wa migogoro ya wakulima na wafugaji.
Mkilanya amesema kuwa Klabu ya waandishi wa habari Morogoro, ina uzoefu katika kushughulikia migogoro ya wakulima na wafugaji kwa njia shirikishi na kuwahi kutekeleza mradi wa elimu shirikishi kwa umma katika utatuzi wa migogoro ya ardhi.