RC Singida ataka wawekezaji adai ardhi inatosha

SINGIDA: MKUU wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego, amewataka wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kujitokeza kuwekeza katika sekta mbalimbali mkoani humo ili kutoa ajira kwa vijana na kuchangia pato la taifa.
Akizungumza Septemba 17, 2025, Dendego amesema mkoa huo una ardhi ya kutosha, nguvu kazi na mazingira rafiki ya uwekezaji bila masharti magumu.
“Mkoa wa Singida uko tayari kwa mapinduzi ya kiuchumi kupitia ushirikiano wa karibu kati ya serikali na sekta binafsi. Uwekezaji katika nishati safi, miundombinu, viwanda, kilimo, biashara na huduma utaboresha maisha ya wananchi na kukuza uchumi wa taifa,” alisema.
Katika hatua inayoonyesha mchango wa sekta binafsi, Kampuni ya Puma Energy Tanzania imezindua kituo kipya cha mafuta mkoani Singida, ikiwa ni sehemu ya mkakati wake wa kupanua upatikanaji wa nishati salama na ya kuaminika nchini.
Kituo hicho, kilichopo katika Ukanda wa Kati, kitawawezesha madereva, wamiliki wa magari makubwa na wafanyabiashara kupata mafuta bora, vilainishi na huduma za kisasa kwa urahisi. Pia kitakuwa na huduma za gym, mgahawa, duka la rejareja, ofisi pamoja na ukarabati na usafishaji magari.
Mkuu wa Biashara wa Puma Energy Tanzania, Benedict Ndunguru, akimwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Fatma Abdallah, amesema
“Uzinduzi wa kituo hiki ni uthibitisho wa dhamira yetu ya kuleta suluhisho za nishati salama na za kisasa karibu na jamii. Zaidi ya urahisi wa upatikanaji, uwekezaji huu utatoa ajira, kuunga mkono wasambazaji wa ndani na kuchangia moja kwa moja maendeleo ya kiuchumi ya Singida. Tupo hapa kwa muda mrefu na tutaendelea kuwasha nguvu za jamii na kuunga mkono mustakabali wa nishati wa Tanzania.”
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Sheria na Mahusiano ya Kisheria na Umma wa Puma Energy Tanzania, Emmanuel Bakilana, amesisitiza kuwa usalama na ubora ndio msingi wa shughuli za kampuni.
“Usalama unabaki kuwa kiini cha kila tunachofanya. Kwa kuchanganya viwango vya kimataifa na utoaji wa mafuta na vilainishi vya ubora wa juu, tunahakikisha wateja wanapata huduma za kuaminika sambamba na huduma zinazowawezesha kufanikisha ndoto na maendeleo yao,” alisema.
Kituo hicho kipya kinatarajiwa kuongeza ajira, kuimarisha fursa kwa wasambazaji wa ndani na kuendeleza shughuli za kiuchumi mkoani Singida kupitia upatikanaji wa nishati ya kuaminika.
Uzinduzi huo unathibitisha dhamira ya Puma Energy ya kupanua huduma zake, kuhakikisha usalama na kuwekeza katika mustakabali wa nishati wa Tanzania.