REA: Wazalishaji wadogo nishati waingiza megawati 23 gridi taifa

Mkurugenzi wa Teknolojia za Nishati Jadidifu wa REA, Advera Mwijage.

WAKALA wa Nishati Vijijini (REA) umesema wazalishaji na waendelezaji wadogo wa nishati nchini wamezalisha na kuingiza kwenye gridi ya taifa zaidi ya megawati 23 za umeme hadi sasa.

Mkurugenzi wa Teknolojia za Nishati Jadidifu wa REA, Advera Mwijage amebainisha hayo hivi karibuni alipozungumza kwenye mahojiano katika Kipindi cha Jambo Tanzania kinachorushwa hewani na Kituo cha Televisheni cha TBC1.

Alisema wazalishaji na waendelezaji hao wadogo nchini wanazalisha nishati ya umeme kwa kutumia teknolojia ya nishati jadidifu na hadi sasa zaidi ya megawati 23 walizozalisha zimeingia kwenye gridi ya taifa.

Advertisement

Alisema wakati Tanzania ni kinara wa masuala ya nishati safi ya kupikia lakini inafanya vizuri kwenye usambazaji wa umeme kwa wananchi na hiyo ni kielelezo kimojawapo cha uwepo wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Nishati (Mission 300) utakaofanyika Januari 27-28, Dar es Salaam katika Ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC).

Kauli mbiu ya mkutano huo ni ‘Kuharakisha Upatikanaji wa Nishati Afrika’ na malengo ya mkutano huo ni kuangazia dhana nzima ya upatikanaji wa umeme kwa wote hususani katika nyakati ambazo viongozi wa Afrika
wanasisitiza matumizi ya nishati safi na salama.

“REA tuna jukumu la kuongeza upatikanaji wa umeme kwa kutumia vyanzo vingine tofauti na vilivyopo sasa, ikiwemo nishati inayozalishwa kwa vyanzo vya asili kama vile jua, upepo, maji na joto ardhi na tunawasaidia wazalishaji wadogo kuwapa ruzuku na hadi sasa wameshazalisha na kuingiza kwenye gridi ya taifa megawati 23,” alisema Advera.

Alisema REA inasambaza umeme maeneo ya vijijini na pembezoni na kuwa kusambaza pekee umeme haitoshi kwani jukumu lao jingine ni kuhakikisha wanaongeza upatikanaji wa umeme kwa kutumia vyanzo tofauti, ikiwemo nishati mbadala.

Alisema serikali kupitia REA kwa kushirikiana na Benki ya Dunia walitoa Sh bilioni 30 kwa ajili ya kuwapa ruzuku waendelezaji hao wadogo wafanye tafiti za miradi ya kuzalisha umeme na kuwasambazia wananchi na pia, kuuza kwenye gridi ya taifa.

Hadi sasa zaidi ya wazalishaji 15 wamenufaika na fedha za mradi huo, ukiwemo Mradi wa Yovi Hydropower mkoani Mogororo ambao ulipata Dola za Marekani 100,000 kuanzisha mradi huo na wanazalisha megawati moja ambayo tayari wameingiza kwenye gridi.

Kuhusu mkutano huo wa M300, Tanzania itanufaika katika sekta ya umeme hasa ikizingatiwa kuwa wakuu wa mataifa hayo wataidhinisha Mpango Mahususi wa Nishati wa Afrika ambao wanakubaliaka kufanya mageuzi yatakayosaidia kufika lengo la upatikanaji wa nishati kwa wote kwa njia za kuaminika, nafuu na endelevu.