REGROW watoa ajira 178 Hifadhi ya Nyerere
MRADI wa Kuboresha Usimamizi wa Maliasili na kukuza Utalii Nyanda za juu Kusini mwa Tanzania (REGROW), umetoa ajira 178 kwa Watanzania kutoka maeneo mbalimbali katika Hifadhi ya Taifa ya Nyerere kunakotekelezwa mradi huo.
Akizungumza ndani ya Hifadhi ya Nyerere juu ya matokeo chanya ya Mradi wa REGROW,Mhando Jambia amebainisha kuwa kati ya ajira hizo, 78 ni za kudumu mpaka mwisho wa mradi huo ambao ulianza Mei 10, 2023 hadi Agosti 13, 2024 na ajira 100 ni za muda mfupi mfupi kulingana na mahitaji ya watu katika sehemu ya kazi za mradi huu.
Mradi huo unahusisha ujenzi wa majengo ya wafanyakazi wa Hifadhi ya Taifa ya Nyerere, eneo la watalii, geti la kuingia na kutokea mbugani Mtemere na nyumba za kulala watalii, ambapo ajira hizo ni tofauti na wale walioajiriwa kwa ajili ya ujenzi wa Kiwanja cha ndege cha Mtemere kilichopo hifadhini humo.
Naye Muuguzi Vaileth Mdotta, anayefanya kazi kwenye utekelezaji wa mradi huo, ameishukuru serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, kwa mradi wa REGROW kwa kuwa unewapatia ajira Watanzania wengi hali inayowawezesha kujimudu kimaisha pamoja na familia zao.