Risasi rangi za mafuta yazua wasiwasi kiafya

DAR ES SALAAM: Wataalamu wa afya nchini Tanzania wameonya kuhusu hatari ya sumu ya risasi inayopatikana katika baadhi ya rangi za mafuta, wakieleza kuwa watoto wadogo, wanawake wajawazito na wafanyakazi wa upakaji rangi ni miongoni mwa makundi yaliyo katika hatari kubwa ya kuathirika.

Kukabiliwa na kemikali hiyo kunaweza kusababisha madhara makubwa kwa afya ya binadamu, yakiwemo kuathirika kwa ubongo, mfumo wa fahamu, figo na mfumo wa uzazi, hali inayozua wasiwasi kuhusu usalama wa bidhaa zinazotumika katika makazi na maeneo ya kazi.

Akizungumza wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Kimataifa ya Kuzuia Sumu ya Risasi yaliyofanyika katika ofisi za Asasi ya Agenda jijini Dar es Salaam, daktari wa Hospitali ya Rufani ya Mkoa ya Amana, Grace Mhando, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha udhibiti wa kemikali hiyo na kufanya tafiti za kitabibu ili kubaini ukubwa wa athari zake kwa wananchi.

Onyo hilo linakuja wakati juhudi za kupunguza matumizi ya risasi katika rangi zikiendelea nchini, licha ya hatua zilizoripotiwa katika kupunguza kiwango cha bidhaa hizo sokoni.

Katibu wa Asasi ya Agenda, Dorah Swai, amesema upimaji wa rangi zinazouzwa nchini umefanyika tangu mwaka 2009 kwa kushirikiana na Serikali, wazalishaji na mashirika ya kimataifa, yakiwemo ILEEN na LEP.

Kwa mujibu wa Swai, juhudi hizo zimechangia kupunguza kiwango cha rangi zenye risasi kutoka asilimia 77 hadi asilimia 13, ingawa amesema bado kuna haja ya kuimarisha udhibiti ili kuhakikisha kemikali hiyo inaondolewa kabisa katika rangi zinazotumika nchini.

Amesema kiwango cha risasi katika rangi za majumbani hakipaswi kuzidi sehemu 90 kwa milioni, huku akizitaka kampuni za uzalishaji na wafanyabiashara kuhakikisha bidhaa zao zinakidhi viwango vya usalama.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kituo cha Taifa cha Kudhibiti Matukio ya Sumu kutoka Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), Yohana Nanai, amesema kubaini athari za risasi kunaweza kuwa changamoto kwa kuwa dalili zake zinafanana na zile za magonjwa mengine.

Amesema vipimo maalumu na uchunguzi wa historia ya kazi za mtu anayedhaniwa kuathirika ni muhimu katika kubaini chanzo cha tatizo na kusaidia hatua zinazofaa kuchukuliwa.

Wito wa wataalamu hao unaweka msisitizo katika kuimarisha usimamizi wa bidhaa za rangi, kuongeza uelewa wa wananchi na kulinda makundi yaliyo katika hatari ya kuathiriwa na sumu ya risasi.

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button