Ruhila; Bustani ya wanyamapori iliyojaa fursa za uwekezaji, utalii

Katika mwendelezo wa makala za vivutio vya utalii vya Mkoa wa Ruvuma, leo HabariLEO linaangazia Bustani ya Wanyamapori ya Ruhila (Ruhila Zoo) chini ya Mamlaka ya Udhibiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Kanda ya Kusini Mashariki ikiwa iko kilometa nane tu kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, katikati ya Manispaa ya Songea.
Awali kabla ya kukabidhiwa kwa Tawa, Ruhila ilikuwa chini ya mamlaka ya mkoa mwaka 1973, baadaye mwaka 1990 ilikabidhiwa kwa Wizara ya Maliasili, Idara ya Wanyamapori na kisha mwaka 2006 ikahamishiwa chini ya Mamlaka ya Mfuko wa Wanyamapori (TWTF) mwishowe mwaka 2017 Tawa wakapewa jukumu la uhifadhi wa eneo hilo ambalo sasa linatumika kwa utalii.
Bustani hiyo imebarikiwa uoto wa asili ikiwemo miti ya miyombo, misukusuku na mipangapanga ambayo imedumu katika eneo hilo kwa miaka 52 bila kubadili asili ya eneo hilo.
Ofisa Mhifadhi wa Tawa anayesimamia bustani hiyo, Daudi Tesha anasema asili ya jina Ruhila ni eneo hilo kupitiwa na Mto mkubwa wa Ruhila katikati yake.
Akifafanua kuhusu maana ya neno hilo, Tesha anasema: “Mto huu ulikuwa na maporomoko huko nyuma kwa hiyo watu wengi walikuwa wakipita sehemu ambazo hazina vivuko walikuwa wanaanguka na kuzama. Kwa hiyo watu wakazoea kusema ‘kuhira’ wakimaanisha kuzama, likatoholewa na kuwa Ruhila. Kwa kuwa mto huu umepita katikati ya bustani hii ikaonekana ipewe jina hili.”
Anasema ndani ya Ruhila Zoo kuna aina mbalimbali za wanyama walioachiwa huru kama vile pundamilia, nyumbu, pofu, swala pala, pongo, digidigi na kuro.
Kwa mujibu wa Tesha, pia wapo wanyama waliowekwa kwenye vizuizi kutokana na ukali wao sambamba na kuruhusu watalii kuwaona kwa urahisi. Wanyama hao ni pamoja na simba, chui, tembo, tausi na chiriku.
Ili kuboresha mazingira ya utalii na kuyafanya yawe ya kuvutia zaidi, anasema Tawa imejenga vibanda vya kupumzika watalii na ukumbi unaowezesha kula na kuangalia runinga ikiwa ni pamoja na kutazama mechi za mpira wakiwa bustanini hapo.
Pia, kuna bwawa la kuogelea na michezo mbalimbali ya watoto ikiwemo kuendesha magari ndani ya bustani hiyo na michezo ya kuendesha baskeli.
Anasema mbali na utalii wa kuona wanyama, watalii wanaweza kufanya utalii wa kambi kwa kuwa kuna eneo maalumu lililowekwa kwa ajili ya watu kuweka mahema, eneo ambalo ni salama lenye huduma zote muhimu za mawasiliano, umeme na maji.
Aidha, anasema eneo hilo ni rahisi kufikika kwa usafiri wa gari, bajaji na pikipiki, gharama za kiingilio zikiwa ni Sh 5,900 kwa mtoto na 11,800 kwa mkubwa huku huduma za ndani zikilipiwa kuanzia Sh 3,000 hadi 10,000 kutegemeana na aina ya huduma (bidhaa) husika.
Tesha anasema asilimia kubwa ya watalii ni wa ndani wengi wao wakitoka ndani ya Manispaa ya Songea wakijumuisha makundi ya wanafunzi wa shule za msingi, sekondari, vyuo pamoja na wafanyakazi wa taasisi mbalimbali.
Anasema kwa sasa wanapokea wastani wa watalii 52 kwa wiki na kuongeza kuwa msimu wenye watalii wengi ni kuanzia Julai hadi Oktoba kwa sababu mvua zinakuwa zimeisha na wakulima wameshamaliza shughuli za kilimo hivyo wana nafasi ya kutosha kutembelea bustani hiyo kwa utulivu.
Mkazi wa Mkuzo katika Manispaa ya Songea, William Shirima anasema amefurahishwa na mazingira aliyokutana nayo katika bustani hiyo na kushauri watu wengine watembelee ili wajionee uzuri wake.
“Nimefurahia mazingira mazuri, wanyama wapo na bei ni nzuri, nawahimiza wengine wafike kufanya utalii wa ndani,” anasema.
Naye Romana Ngonyani anasema: “Nimefurahia hifadhi (bustani) hii nzuri wanyama wamenivutia hasa simba na watoto wake wamefurahisha sana.”
Fursa za uwekezaji
Akizungungumzia fursa za uwekezaji zilizopo bustani hiyo, Tesha anasema zipo nyingi na wameandaa maeneo maalumu kwa ajili ya uwekezaji.
“Tunakaribisha wawekezaji wa mahoteli, tuna eneo zuri tumeliandaa kwa ajili hiyo ambalo mtu akikaa anaweza kuona bustani yote kutokea hapo,” anasema.
Aidha, anasema lipo eneo lililoetengwa kando ya Mto Ruhila kwa ajili ya uwekezaji wa mahema, hivyo mtu yeyote aliye tayari kuwekeza anaweza akatumia fursa hiyo akaweka mahema watalii wakafika na kulala.
Anasema katika hilo, hata utalii wa uvuvi pia utashamiri.
Anasema uwekezaji mwingine ni miundombinu ya utalii wa kutembea na vitoroli kwenye waya kutokana na eneo lilivyo na bonde lililotokana na Mto Ruhila na miti mikubwa iliyoko pembezoni.
Katika hatua nyingine, Tesha anakaribisha wawekezaji wa huduma za chakula na vinywaji katika ukumbi uliojengwa na Tawa katika bustani hiyo.
Kuhusu uboreshaji wa huduma anasema Tawa ina mikakati ya kuongeza wanyamapori hasa wale watakaowezesha watalii kupiga nao picha na kuwalisha chakula wakiwa vile twiga, swala, pofu na mbuni.
Aidha, anasema upo mkakati utakaoanza kufanyiwa kazi hivi karibuni wa kufanya utalii wa kutembea.
Kwa mujibu wa Ofisa Mhifadhi huyo, Tawa watakuwa na vizimba vinavyotembea na kutoa fursa kwa watu wasio na muda wa kutembelea hifadhi waweze kuona wanyama mbalimbali wakiwa kwenye maeneo yao.
Anasema anajivunia kuona eneo hilo likiendelea kubaki na asili yake kwa miaka yote 52 na anajivunia jamii ya wana Songea ambao wamekuwa tayari muda wote kuhakikisha uhifadhi katika eneo hilo unakuwa endelevu.
“…Niwashukuru wananchi wa Songea, wametuunga mkono kwa kiasi kubwa, kwa hali iliyopo hapa hatuna matatizo mengi ya uvamizi, si kwa sababu sisi ni mabingwa wa kulinda! Ni sapoti yao kubwa imechangia,” anasema.
Anaongeza, “Wamechukulia chanya na wengi wao wanaona eneo hili ni lao, ndiyo maana hatujawahi kupata kesi ya wananchi kuingia kuwinda au kukata miti, kwa hiyo uhifadhi wetu unategemea sana wananchi na tunawashukuru sana.”
Aidha, anasema kwa juhudi na uwekezaji unaofanywa na serikali katika sekta ya utalii mkoani Ruvuma, anaiona mbali Ruhila miaka mitano ijayo.
“Miaka mitano ijayo Ruhila itakuwa juu sana, kama ndoto zetu tulizonazo zitatimia, tutakuwa mbali. Nataka kuona ukimuuliza mtu Ruhila Zoo anaifahamu akiwa Kampala, anaifahamu akiwa Kigali na kwingineko, nataka itanuke hivyo,” anasema