Ruwa’ichi: Hatushindani na serikali

ASKOFU Mkuu wa Jimbo Kuu la Kanisa Katoliki Dar es Salaam, Jude Thaddaeus Ruwa’ichi amesema Kanisa Katoliki halina mpango wa kushindana na serikali.

Askofu Mkuu Ruwa’ichi amesema hayo Dar es Salaam alipokuwa akihitimisha adhimisho la misa takatifu ya jubilei ya mapadre wa jimbo hilo lililofanyika katika Parokia ya Bikira Maria wa Fatima Msimbazi.

“Kwa hiyo, wale wanaohangaika wakidhani kwamba Kanisa Katoliki linataka kushindana, kulumbana au kushikana mieleka na serikali, watambue kwamba sisi hatuna mpango huo,” amesema.

SOMA: Ruwa’ich akemea kutegemea sangoma badala ya Mungu

Askofu Mkuu Ruwa’ichi amesema siku za hivi karibuni kumekuwa na tangazo linalosambaa kwenye mitandao ya kijamii, likionesha kwamba warsha ya waumini katika jimbo hilo itafanyika Oktoba 29, mwaka huu ambayo ni siku ya Uchaguzi Mkuu, taarifa ambayo si ya kweli.

Amesema tangazo hilo halikutolewa na ofisi yake, hivyo watu wanapaswa kutambua kuwa si tangazo rasmi.

“Naomba nitamke kwamba tangazo hilo halikutolewa na ofisi yangu, kwa hiyo si tangazo linalobeba saini yangu au lililotangazwa kupitia kwa katibu mkuu.

Hilo liwafanye kutambua kwamba siyo tangazo rasmi, jambo lililotangazwa kwamba litafanyika Oktoba 29, katika kalenda yetu ya jimbo limepangwa kufanyika Novemba 29, mwaka huu,” amefafanua.

Amewataka watu kuyachunguza vizuri matangazo yanayotolewa na mitandao na vyombo vya habari.

“Kwa hiyo, tamko hili langu liwasaidie muwe na uelewa sahihi na mfuate msimamo sahihi. Mnapoona matangazo yametolewa kwenye vyombo vya habari kayachunguzeni vizuri kabla hamjaanza kuhaha, maana siku hizi kumekuwa na kuhaha kwingi na huko ni kutokana na kutokuwa makini kutokana na kutochambua na kubainisha uhalisia wa jambo linalotangazwa,” amesema Askofu Mkuu Ruwa’ichi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button