Ruwasa kupeleka maji vijiji vyote Kigoma

KIGOMA: WAKALA wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) mkoani Kigoma imejizatiti kuhakikisha majisafi na salama yanapatikana kwa uhakika kwenye vijiji vyote mkoani Kigoma.
Meneja wa RUWASA Kigoma, Mhandisi Mathias Mwenda amesema hayo katika mafunzo ya siku nne kwa watendaji waandamizi wa wakala huo kutoka wilaya zote za mkoa huo mafunzo yaliyoandaliwa na shirika lisilo la kiserikali la Water Mission kwa ufadhili wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF).
Mwenda amesema upatikanaji maji vijijini mkoani Kigoma umefikia asilimia 72 na kwamba kuna miradi 25 ambayo inatekelezwa ambapo kukamilika kwake kutafanya upatikanaji maji vijijini mkoani humo kufikia asilimia 85.

Akizungumza katika siku ya kwanza ya mafunzo hayo, Ofisa Maendeleo ya Jamii wa Shirika la Water Mission walioandaa mafunzo hayo, Rose Mlela amesema kuwa mafunzo hayo yanalenga kubadilishana uzoefu wa namna ya usanifu na utekelezaji wa miradi kwa kutumia mfumo wa umeme jua na kuifanya miradi hiyo kuwa endelevu na kuweza kuyoa huduma wakati wote.
SOMA ZAIDI: Ruwasa wajipanga kupunguza adha ya maji Geita
Awali Mkuu wa ofisi ya UNICEF mkoa Kigoma, Justus Ndenzako alisema kuwa mafunzo hayo yanawaweka pamoja na kuwajengea uwezo wahandisi na wasimamizi wa miradi inayotekelezwa ili miradi ikamilike kwa viwango, ianze kutoa huduma lakini pia miradi iweze kudumu kwa muda mrefu na kutimiza lengo la kusogea maji karibu na wananchi na kuondoa kero ya kutafuta maji umbali mrefu.



